T-MOTO WAPATA KIBALI BASATA


KUNDI jipya la muziki wa taarab hapa nchini, Tanzania Modern Taarab ‘T-Moto’, limepata usajili rasmi kutoka kwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha kujihusisha na sanaa hiyo ndani na nje ya nchi.
Kundi hilo limepewa namba ya usajili EST, 4735 iliyotolewa Septemba 27, mwaka huu hali ambayo itaongeza chachu ya kufanya mambo makubwa zaidi katika kampeni yao ya kuyafunika makundi mengine ya muziki huo hapa nchini na kwingineko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa na Mkurugenzi wa kundi hilo, Amin Salmin ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Salmin Amour, kwa sasa wanamuziki na wasanii wa kundi hilo wamepata nguvu mpya baada ya kutambulika rasmi na serikali.
Aliahidi kundi lake kutoa burudani ya nguvu kwa wapenzi wa taarab nchini kwani wamepania kundi hilo kuwa tofauti na makundi mengine yaliyopita kutokana na kujiandaa vilivyo.
“Kwanza kabisa napenda kutoa shukurani zangu kwa BASATA kwa kutupokea, lakini pia ningependa kuwaahidi wapenzi wa taarab Tanzania Bara, Visiwani na kwingineko kuwa hatutawaangusha hata kidogo katika suala zima la utoaji wa burudani inayolingana na hadhi yao.
Kundi hilo limeshaingia Studio za Bakunde Production zilizopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam kurekodi nyimbo zake mpya zilizokamilika ili kukamilikamisha albam yao ya kwanza itakayojulikana kwa jina la Aliyeniumba Hajanikosea.
Baadhi ya wasanii wanaounda kundi hilo ni kiongozi Jumanne Ulaya ‘Mkono wa Biashara’, Mwanahawa Ally, Jokha Kassim, Mrisho Rajab, Musa Mipango, Hassan Ally, Mosi Suleiman, Rajab Kondo, Fadhili Mnara, Moshi Mtambo, Ally Kabura, Sabha, Rahma, Asha Masanja na Hanifah Kasim na wengineo.
Nyimbo za kundi hilo ambazo zimeshakamilika ni Aliyeniumba Hajanikosea uliobeba jina la albam ambao umeimbwa na Mwanahawa, ‘Unavyojidhani Mbona Hufanani’ (Jokha), ‘Mtoto wa Bongo’ (Hassan Ally), ‘Mchimba Kaburi Sasa Zamu Yake Imefika’ (Rajab), ‘ Mwenye Kustiri Mungu’ na ‘Kumbe Wewe ni Shoti’ (Mosi) na ‘Riziki na Shortcut’ (Aisha).

Comments