T- MOTO MODERN TAARAB WAREJEA DAR

KUNDI jipya la muziki wa taarab la T-Moto Modern Taarab lililokuwa Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujinoa, limewasili jijini Dar es Salaam leo na kesho linatarajiwa kuingia studio kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake zilizosalia ili kukamilisha albamu yao.

 Mkurugenzi wa kundi hilo Amin Salmin alisema kwamba kundi hilo litaingia katika stuio za Bakunde na kurekodi nyimbo sita ambazo zitakamilisha albamu yao hiyo iitwayo ‘Aliyeniumba Hajanikosea’.
Alisema kuwa mara baada ya kumaliza zoezi la kurekodi nyimbo hizo, kundi hilo linatarajiwa kufanya ziara mikoani na Nairobi, Kenya kabla ya kufanya rasmi uzinduzi wakundi na albamu Oktoba 28, jijini Dar es Salaam.
Mmoja ya wasanii wa kundi hilo, Mwanahawa Ally alisema anashukuru kambi hiyo imewaweka katika mwelekeo mzuri ambapo anaamini kazi zitakazotoka zitakuwa na viwango vya hali ya juu hivyo amewaomba mashabiki wakae mkao wa kula.
“Nataka niwaeleze mashabiki wa tasnia ya taarab kwamba tunakuja kwa moto wa hali ya juu hivyo wasubiri mambo mazuri na ya kupendeza kutoka kwetu, tunawaomba mashabiki watupokee vizuri kwa kujitokeza kwa wingi katika maonyesho yetu,”Alisema.
Tayari kundi hilo limeshatoa nyimbo mbili ambazo zimeweza kulitambulisha vema.Nyimbo hizo ni pamoja na huo uliobeba jina la albamu ‘Aliyeniumba Hajanikosea’ ulioimbwa na Mwanahawa Ally, pamoja na ‘Unavyojidhani Mbona Hufanani’ ulioimbwa na Jokha Kassim.
Nyimbo nyingine zinazotarajiwa kuwemo katika albamu hiyo ni pamoja na ‘Mtoto wa Bongo’ ulioimbwa na Hassan Ally, ‘Mchimba Kaburi Sasa Zamu yake imefika’ ulioimbwa na Mrisho Rajab, ‘ Mwenye Kustiri Mungu’, ‘Kumbe Wewe ni Shoti’ ambazo zimeimbwa na Mosi Suleiman na ule wa ‘ Riziki na Shortcut’ uliombwa na Aisha Masanja.
Kundi hilo limesheheni wasanii wenye vipaji vya hali ya juu wakiwemo Mwanahawa Ally, Jokha KAssim, Jumanne Ulaya ‘Mkono wa Biashara’, Mrisho Rajab, Musa Mipango, Hassan Ally, Mosi Suleiman, Rajab Kondo, Fadhili Mnara, Moshi Mtambo, Ally Kabura, Sabha, Rahma , Asha Masanja na Hanifah Kasim na wengineo.

Comments