STARS YABANWA NYUMBANI, YATOKA SARE YA 1-1 NA ALGERIA


MATUMAINI ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kushiriki fainali za mataifa ya Afrika mwakani leo yalififia baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na Ageria katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo Stars iliyopo kundi D inabakia katika nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi tano na kuambulia pointi tano sawa na Algeria wakati Afrika ya Kati na Morocco wanaomenyana kesho  tayari kila moja ilikuwa na pointi saba.Ikiongozwa na wachezaji wake wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiwemo Samata, Nizar, Danny Mrwanda, Abdi Kassim na Henry Joseph Stars itabaki ikijilaumu kwa kushindwa kutumia vema nafasi za wazi ilizozipata katika mechi hiyo.
Wapinzani wao nao licha ya kusheheni nyota wanaokipiga barani Ulaya lakini walishindwa kufurukuta dhidi ya Stars ambapo walishindwa kuonyesha kiwango cha juu kama ilivyotarajiwa kwa timu yenye nyota wengi wa kulipwa.
Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa na upinzani mkubwa, Stars ilianza kutikisha nyavu za Algeria kupitia kwa Mbwana Samata aliyefunga kwa mguu wa kushoto katika dakika ya 21baada ya kupokea pasi ya Nizar Khalfani.
Samata alionekana mwiba mchungu kwa mabeki wa Algeria kwani aliweza kuiandama ngome ya Algeria mara kwa mara lakini walijiimarisha kuhakikisha hapati nafasi ya kucheka na nyavu zao.

Comments