SIMBA, TOTO AFRICANS WAINGIZA MIL.24

Pambano namba 44 la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Toto Africans na Simba lililochezwa Septemba 21 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza limeingiza sh. 24,044,000. Viingilio katika mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3 vilikuwa sh. 2,000 kwa mzunguko na sh. 10,000 kwa jukwaa kuu.
LIGI DARAJA LA KWANZA
TIMU saba kati ya 18 za Ligi Daraja la Kwanza bado hazijawasilisha usajili wao wakati ligi hiyo inatarajia kuanza mapema mwezi ujao. Timu hizo ni Temeke United, 94 KJ, Polisi Morogoro, Samaria FC, Rhino FC ya Tabora, Morani FC ya Manyara na AFC ya Arusha. Ingawa timu kumi na moja zimewasilisha usajili wao, lakini ni sita tu ambazo zimelipa ada ya ushiriki ya sh. 200,000. Timu zilizolipa ni Polisi Iringa, Burkina Faso ya Morogoro, Mlale JKT ya Ruvuma, Morani FC ya Manyara, Mgambo Shooting, Samaria FC na Transit Camp.
Timu nyingine za Daraja la Kwanza ni Polisi Dar es Salaam, Tanzania Prisons, Mbeya City Council, Polisi Tabora, Small Kids ya Rukwa na Majimaji.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Comments