SIMBA SC YALIINGIA CHAKA LIGI KUU

SARE mfululizo walizozipata vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, katika michezo yake ya hivi karibuni, zinadhihirisha kuwa timu hiyo sasa imeingia rasmi kwenye ligi.

Hiyo inatokana na awali kukutana na timu nyepesi zikiwemo zile ambazo zimepanda daraja msimu huu kama JKT Oljoro, Coastal Union, Villa Squad na Polisi Dodoma na kufanikiwa kuvuna pointi 12 baada ya kushinda mechi zake zote.
Hata hivyo, Simba walianza kukutana na ushindani kwenye ligi hiyo baada ya kukutana na Kagera Sugar, Azam na Toto African ambapo waliponea chupuchupu kufungwa kabla ya kulazimisha sare.
Simba ambayo inashuka keshokutwa katika dimba la Taifa kukwaana na Mtibwa Sugar ya Morogoro ambayo msimu huu inaonekana kuimarika kiasi cha kukimbilia kwa kasi usukuni wa ligi hiyo.
Kwa mantiki hiyo, mechi ya Simba na Mtibwa itakuwa na upinzani mkubwa kwani kila timu itataka kudhihirisha umahiri wake sambamba na kutaka kushinda ili kujipatia pointi tatu.
Aidha, Simba ambayo bado haijacheza na timu kama JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Moro United, Yanga na African Lyon kama itashinda mechi hizo itadhihirisha kuwa mwaka huu imejiandaa kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Mpaka sasa Simba inaongoza ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba huku ikishinda minne na kutoka sare mitatu, inafuatiwa na Azam yenye pointi 14 na Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 12.

Comments