SALHA ISRAEL NDIYE MISS TANZANIA 2011




HATIMAYE ngebe za kanda ipi itafanikiwa kutwaa taji la Vodacom Miss Tanzania mwaka 2011/2012 zilimalizwa usiku wa kuamkia leo baada ya mrembo kutoka Kanda ya Ilala,Salha Israel kunyakua taji.

Salha alitwaa taji hilo baada ya kuwashinda wenzake 29 waliotinga fainali za shindano hilo zilizohitimishwa katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Salha ambaye ataiwakilisha Tanzania katika fainali za Miss World zitakazofanyika baadaye huko London, Uingereza, alizawadiwa gari aina ya Jeep Patriot lenye thamani ya shilingi mil.72, pamoja na fedha taslimu shilingi mil.nane.
Mrembo huyo ambaye anashikilia taji la Kitongoji cha Dar City Centre, licha ya kutokuwa midomoni mwa watu kama ilivyokuwa kwa wengine, alidhihirisha ubora wake katika hatua ya tano bora baada ya kuweza kujibu kwa ufasaha na kwa kujiamini swali aliloulizwa.
Salha alitinga hatua ya tano bora pamoja na Tracey Sospeter mrembo kutoka Shinyanga aliyekuwa wa pili, Alexia William kutoka Dar City Centre (Ilala) aliyekuwa wa tatu, Jennifer Kakolaki kutoka Dar City Centre (Ilala) na Loveness Flavian kutoka Lindi aliyekuwa wa tano.
Mshindi wa pili katika mashindano hayo alizawadiwa shilingi mil.6.2, mshindi wa tatu alipata shilingi mil.nne, mshindi wan ne alizawadiwa shilingi mil.tatu, mshindi wa tano aliondoka na mil.2.5, wakati mshindi wa 6-15 kila mmoja alizawadiwa shilingi mil.mbili, huku mshindi wa 16-30 kila mmoja alipata shilingi 700,000.
Aidha, katika mashindano hayo kulikuwa na washindi wa mataji madogo madogo ambao walitinga 15 ya fainali hizo,Mwajabu Juma (Miss Top Model), Tracey Sospeter ( Miss Photogenic), Loveness Flavian ( Miss Sports Woman), Rose Hurbert ( Miss Talent) na Alexia William aliyetwaa taji la Miss Personality.
Washiriki wengine waliotinga 15 bora ni Jenniffer Kakolaki, Stella Mbuge, Mariaclara Mathayo, Cynthia Kimasha, Irene Karugaba, Christina William, Chiaru Masanobo,Hamisa Hassan, Salha Israel na Stacey Alfred.
Katika shindano hilko lililodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, kulipambwa na burudani toka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo Juliana Kanyomozi wa Uganga, Bob Junior, Diamond, Michael Jackson wa Tanzania na Akili the Brain

Comments