POULSEN AWEKA TUMAINI KWA COSTA

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Jan Poulsen amemmwagia sifa beki wake mpya wa timu hiyo, Victor Costa Nampoka 'Nyumba' akisema mchezaji huyo ni jibu la matatizo ya safu ya ulinzi. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Poulsen alisema beki huyo ana uwezo mkubwa na kwamba ataisaidia timu hiyo katika mechi zake zilizobaki.

Stars inakabiriwa na mechi ngumu ya kuwania nafasi ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika AFCON dhidi ya Algeria siku ya Jumamosi katika pambano litakalopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katika pambano hilo kila timu inahitaji ushindi ili iweze kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwa kuwa timu hizo mbili zimefungana kwa pointi nne katika Kundi D.

“Costa ni beki mwenye nguvu, akili, pamoja na uzoefu hivyo ninaamini kwamba ataisaidia timu yangu ingawa bado hajaweza kwenda sambamba na mbinu pamoja na mfumo ninaofundisha,” alisema Poulsen.
Alisema,“Ninajitahidi kumweka sawa kabla ya kukutana na Algeria siku ya Jumamosi na kinachonifurahisha zaidi ni umakini wake kila ninapojaribu kumwelekeza anaelewa na kuyafanyia kazi ndiyo maana ninasema kuwa ni jibu katika timu yangu.”

Poulsen alisema Costa ni mchezaji asiyekuwa na papara katika kufanya uamuzi na kwamba hiyo ndiyo moja ya sifa ya beki mzuri katika timu. Katika hatua nyingine Poulsen alisema washambuliaji wa timu hiyo bado hawajaelewana ipasavyo na pengine hiyo inatokana na timu wanazochezea kuwa na viwango tofauti vya soka.

Hata hivyo kocha huyo hakutaka kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja, lakini akafafanua kuwa siku chache zilizobaki zinamtosha kuwaweka pamoja kwa sababu siyo mara yake ya kwanza kuwa nao na wanaelewa mbinu na mfumo wake wa ufundishaji. Mpaka sasa kikosi cha Taifa Stars kimepoteza mechi mbili katika mechi nne kilichocheza mpaka sasa katika kutafuta nafasi ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 2012 huko nchini Gabon na Guinea ya Ikweta.

Mechi ya mwisho Taifa Stars ilishindwa kutamba mbele ya timu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya kuchapwa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Barthelemy Boganda mjini Bangui.
Kutokana na kupoteza mechi hiyo Taifa Stars hivi hivi sasa ipo katika nafasi ngumu ya kufuzu kushiriki fainali hizo za Afrika, ambapo imebakisha mechi mbili ambazo inatakiwa kushinda mechi zote ili ifikishe pointi 10.

Taifa Stars imebakisha mechi dhidi ya Algeria ambayo itachezwa jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa Septemba 3, pia imebakisha mechi dhidi ya Morocco ambayo itachezwa huko mjini Rabat kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah kati ya tarehe 7,8,9/10/2011. Wakati huohuo; Mabingwa watetezi Misri na vigogo wenzao Cameroon wapo kwenye hatari ya kushindwa kufuzu kushiriki Fainali za Afrika za mwakani.

Wakati harakati za kufuzu kushiriki fainali hizo zikitegemewa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki, timu hizo mbili za Afrika kati ya tatu zilizotwaa taji hilo mara nyingi zaidi hazitegemewi kuwapo katika fainali zitakazofanyika kwenye nchi za Gabon na Guinea ya Ikweta. Mabingwa mara mbili Nigeria pia wapo njia panda. Hata Ghana iliyocheza robo Fainali za Kombe la Dunia 2010 bado ina kazi ya kufanya. 

Tofauti na nchi kama Morocco, Tunisia na Mali zenyewe zitaweza kuungana na Jamhuri ya Afrika Kati, Malawi na Cape Verde kwenye fainali za mwakani.

Comments