NANI KUVAA VIATU VYA GENEVIEVE MPANGALA, JEEP PATRIOT LEO?

 GENEVIEVE EMMANUEL MPANGALA,MISS TANZANIA ANAYEVUA TAJI LEO
HUU MCHUMA AINA YA JEEP PATRIOT WENYE THAMANI YA SHILINGI MIL.72 ATAZAWADIWA MSHINDI

WAREMBO 30 kutoka kanda mbalimbali hapa nchini, leo wanatarajiwa kupanda jukwaani kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, katika fainali za shindano la kuwania taji la Vodacom Miss Tanzania 2011.
Warembo hao ambao wamekuwa kambini kwa wiki kadhaa sasa, wakianzia katika hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam na baadaye kwenye jumba maalum lililojulikana kama ‘Vodacom House’, watakuwa katika mchuano mkali wa kumrithi mrembo wa mwaka jana, Genevieve Emmanuel Mpangala, ambaye leo anavua taji.
Chini ya udhamini wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, warembo hao wakiwa kambini, walipata kujifunza masuala kadhaa ya kijamii, sambamba na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, pia kufanya shughuli za kijamii.
Kama ilivyo ada, mashindano hayo kila mwaka huwa na upinzani mkali, ukihusisha kanda kutokana na kila eneo kuwa limejipanga vema kwa kutafuta warembo wenye sifa na vigezo vinavyostahili, ili kuhakikisha wananyakua taji.
Wakati taji hilo likiwa linashikiliwa na Kanda ya Temeke, lakini Kanda za Ilala, Kinondoni, Nyanda za Juu Kusini, Ziwa, Kaskazini, Elimu ya Juu, Kati na Mashariki, nazo zimepania mwaka huu kuhakikisha zinatwaa taji hilo.
Hata hivyo, kabla ya fainali za leo, kulifanyika mashindano ya kuwania mataji madogo yaliyofanyika kwa nyakati tofauti, ambako washindi wake walikata tiketi ya kutinga moja kwa moja hatua ya nusu fainali ya shindano hilo, ambayo itahusisha warembo 15 badala ya 10 ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Warembo ambao tayari wametinga nusu fainali na mataji yao kwenye mabano ni pamoja na Mwajabu Juma (Top Model), Rose Albert (Talent), Tracy Mabula (Miss Photogenic), Loveness Flavian (Top Sports Woman), na Alexia William (Miss Personality).
Mbali na warembo hao, washiriki wengine wa shindano hilo ni pamoja na Chiaru Masonobo, Zerulia Manoko, Maua Kimambo, Dalilah Ghalib, Christine Mwenegoha, Chritine William, Atu Daniel, Leyla Juma, Zubeda Seif, Stacey Alfred, Husna Twalib, Cynthia Kimasha, Neema Mtitu, Weirungu David, Glory Lory, Blessing Ngowi, Asha Salehe, Mariaclara Mathayo, Irene Karugaba, Glory Samwel, Stella Mbuge, Husna Maulid, Hamisa Hussein, Salha Israel na Jenifer Kakolaki.
Aidha, mshindi katika shindano hilo atazawadiwa gari jipya aina ya Jeep Patriot lenye thamani ya sh milioni 72, pamoja na fedha taslim milioni 8, huku mshindi wa pili atajitwalia fedha taslim shilingi milioni 6.2, wakati wa tatu atapata shilingi milioni 4.
Mshindi wa nne, ataondoka na shilingi milioni 3, wa tano atapata shilingi milioni 2.4, wakati wa sita hadi 15 kila mmoja atapata milioni 2 wakati wa 16-30 kila mmoja atapata kifuta jasho cha shilingi 700,000.
Tangu kuanza kwa shindano hili mwaka 1994, taji lilinyakuliwa na Aina Maeda, Emily Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basila Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999), Jacquiline Ntuyabaliwe (2000), Happiness Magese (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003), Faraja Kotta (2004), Nancy Sumari (2005), WEma Sepetu (2006), Richa Adhia (2007), Nasreen Karim (2008), Miriam Gerald (2009) na Genevieve Mpangala (2010).

Comments