MISS TANZANIA 2011 KUONDOKA NA JEEP PATRIOT YENYE THAMANI YA SHILINGI MIL.72



WAKATI shindano la kumsaka Vodacom Miss Tanzania mwaka 2011 likitarajiwa kufanyika jumamosi katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, mrembo atakayetwaa taji hilo atazawadiwa gari aina ya Jeep Patriot lenye thamani ya shilingi mil.72, pamoja na fedha taslimu shilingi milioni nane.
Akizungumza katika hafla ya kutangaza zawadi kwa washiriki wa mwaka huu, mkuu wa udhamini wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom George Rwehumbiza alisema kwamba kampuni yake inajisikia fahari kudhamini shindano hilo lenye hadhi ya juu kuliko mashindano yote ya urembo hapa nchini.
Alisema kama wadhamini wakuu wa shindano hilo wamekuwa wakiboresha kila mwaka udhamini wao kwani mwaka jana mrembo aliyetwaa taji hilo alizawadiwa gari aina ya Hyundai i10 lenye thamani ya shilingi mil.12.
“Ni matumaini yangu gari hili litamrahisishia usafiri wa mrembo wetu kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kama litatumika ipasavyo litachangia kumletea maendeleo kwa kuweza kutekeleza shughuli zake za kijamii kwa wakati,”Alisema.
Aidha, Rwehumbiza alisema mshindi wa pili atazawadiwa shilingi mil.6.2, mshindi wa tatu atapata shilingi.mil.4.5, mshindi wan ne ataondoka na shilingi mil.3 na wa tano atapata shilingi mil.2.4, huku mshindi wa 6-15 kila mmoja atapata shilingi mil.2 na mshindi wa 16-30 kila mmoja ataondoka na shilingi 700,000.
Naye mkurugenzi wa Lino International Agency inayoandaa shindano hilo Hashim Lundenga aliwashukuru Vodacom kwa kuthamini mashindano hayo kwani warembo wamekuwa wakipitia safari ndefu mpaka kufikia fainali, hivyo kwa kuwapa zawado inayoendana na changamoto wanazokumbana nazo inawatia moyo na kufanya vema katika mashindano ya kimataifa.
Warembo 30 ambao kwa sasa wapo katika kambi maalum ‘Vodacom House’ wakiendelea na mazoezi ya kujiandaa na shindano hilo ambapo mrembo anayeshikilia taji hilo, Geneviev Mpangala ndiye mkufunzi wa warembo hao.

Comments