MICHUANO YA AIRTEL RISING STARS YAANZA KUTIMUA VUMBI

 Mchezaji Jimmy Michael (kushoto) wa timu ya Mkoa wa Morogoro, akijiandaa kupiga mpira huku akikabwa na Moses Joseph wa timu ya Mwanza, katika mechi ya ufunguzi wa michuano ya vijana ya Airtel Rising Stars ngazi ya Taifa, jana kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.


 Mchezaji Mzamiri Yasin (kushoto) wa Morogoro akiwania mpira na Hussein Majimoto wa timu ya Mwanza, katika mechi ya ufunguzi wa michuano ya kusaka vijana kwa vijana ya Airtel Rising Stars, jana kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mchezaji Ibrahim Hussein (katikati) wa timu ya Morogoro, akitafuta mbinu za kuwatoka wachezaji wa timu ya Mwanza, katika mechi ya ufunguzi wa michuano ya kusaka vijana kwa vijana ya Airtel Rising Stars, jana kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh Kassim Majaliwa, akipiga mpira kuashiria uzinduzi rasmi wa michuano ya Airtel Rising Stars ngazi ya Taifa katika Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi, 17 Septemba mwaka huu.

Timu kombaini ya Morogoro imeifundisha timu ya Mwanza jinsi ya kucheza soka baada ya kuichapanga 5-0 kwenye mechi ya ufunguzi wa michuano ya Airtel Rising Stars iliyochezwa Jumamosi.
Mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Karume Dar es Salaam, ilishuhudia Mwanza wakianza kwa kasi na dakika ya pili tu ya mchezo, kipa wa Morogoro Rajabu Athumani alilazimika kufanya kazi ya ziada na kupangua shuti kali kutoka kwa Samir Omary wa Mwanza. Hata hivyo, Baada ya dakika tano za mchezo, Mwanza walionekana kupoteana kabisa na hivyo kuwapa nafasi Morogoro ambao walianza kutawala uwanja mpaka mwisho wa mchezo na laiti washambuliaji wa Morogoro wangekuwa makini, uwezekano wa kushinda kwa idadi zaidi ya magoli ulikuwapo.
Timu ya Morogoro ilianza kuhesabu karamu ya mabao dakika ya 30 ya mchezo baada ya Kassim Jurugu kuunganisha vyema mpira wa kona kutoka kwa Ibrahim Hussein. Baada ya bao hilo, Mwanza walionekana kuishiwa nguvu kabisa na mnamo dakika ya 32 na 35, washambuliaji wa Morogoro Kassim Jurugu na Graham Naftali walikosa mabao ya wazi kabisa. Hata hivyo, dakika ya 37, Ibrahim Hussein aliwainua tena mashabiki wa Morogoro baada ya kuiandikia timu yake bao la pili. Dakika tatu baadaye, Mwanza wakiwa bado hawakaa vizuri, Kassim Hussein ambaye kwa hakika ndiye alikuwa nyota ya mchezo, aliongeza bao la tatu baada ya kutumia vyema makosa ya kipa wa Mwanza wa kuutema mpira na yeye kumalizia. Mpaka timu zinakwenda mapumziko, Morogoro walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
Katika kipindi cha pili, Mwanza walifanya mabadiliko ambapo Francis Msingi na Jackson Joseph walitoka na nafasi zao kuchukuliwa na Seif Juma na Benedict James. Hata hivyo, hilo halikuzuia Morogoro kuendelea na sherehe yao ya kuvuna magoli kwani dakika ya 54, Ibrahim alifunga bao ya nne kwa timu yake na la tatu kwake mwenyewe. Dakika ya 63, Graham Naftali lifunga goli la tano baada ya kupata pasi murua kutoka kwa Hamis Mwande. Dakika ya 70, Morogoro walifanya mabadiliko ambapo Graham Naftali na Hamis Mwande alitoka na nafasi zao kuchukuliwa na Jimmy Michael na Nassoro Hamza. Mabadaliko hayo hayakusaidia chochote kwani mpaka dakika ya mwisho Morogoro walikuwa na 5 huku Mwanza wakiwa hawajapata kitu. Michuano hiyo inaendelea Jumapili ambapo Dar es Salaam itamenyana na Iringa.
Wakati wa ufunguzi wa michuano hiyo ambapo Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh Kassim Majaliwa, alipongeza kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kuwekeza kwenye soka la vijana na kuhaidi ushirikiano kutoka kwa serikali. Pia alitoa changamoto kwa kampuni kufikia mikoa mingine zaidi hapo mwakani.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Jackson Mmbando aliwapongeza wachezaji walichanguliwa kucheza fainali ya michuano hiyo. Alitoa wito kwa wachezaji hao kuongeza bidii kwani wakati wa michuano hiyo, wachezaji sita bora watachanguliwa kujiunga na kambi maalum ya Kimataifa ambayo itafanyika hapa nchini, ikiwa chini ya waalimu wa soka kutoka klabu ya Manchester United ya Uingereza.

Comments