MHINA PANDUKA MATATANI

MWIMBAJI maarufu nchini Tanzania, Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ ameingia matatani baada ya uongozi wa bendi ya K-Mondo Sound kuamua kumfungulia kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.


Taarifa iliyotolewa na Menejimenti ya K-Mondo na kusainiwa na Meneja wa bendi hiyo Connie Karanja ‘Aunt Connie’ imesema imefikia hatua ya kumshitaki Panduka baada ya kujaribu kumuita mara kadhaa tangu Aprili mwaka huu kutaka kumaliza suala lake lakini mwanamuziki huyo kuonekana jeuri.
“Tulimwita Panduka Aprili mwaka huu wakati wa sikukuu ya Pasaka aje kumaliza suala la mkataba wake, Panduka alisaini mkataba wa kufanya kazi na bendi yetu wa mwaka mmoja tangu Oktoba mwaka jana lakini alifanya kazi kwa mwezi mmoja akatimikia Zanzibar baadae akawa yuko TOT, tulipozungumza nae alisema hajasaini mkataba na TOT na atarudi, lakini akaomba afanye shoo ya Jumapili ya Pasaka pale Mango na TOT halafu atarudi lakini mpaka leo hajatokea,

Tulimuandikia barua kupitia kampuni ya uwakili ya JM Attorney na akatakiwa kumaliza suala hili lakini mpaka leo hakuna alichojibu zaidi ya kuwatumia meseji viongozi kuwa watapambana mahakamani,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema wanamuziki wengine watatu ambao walikuwa wamechukua pesa na kukimbia wote waliamua kurudi kumalizia mikataba yao na mwingine ambaye ni mpiga rythim Fadhili aliamua kurudisha hela. Wengine waliokuwa wameondoka baada ya kuchukua hela lakini wakaamua kurudi kumalizia mikataba yao ni Joshua Bass ambaye alikuwa ameenda THT na Husein Said Tumba aliyekuwa ameenda Royal.

Taarifa iliongeza kuwa baada ya kushauriana na wanasheria uamuzi uliofikiwa ni kumfungulia kesi hiyo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ili sheria ichukue mkondo wake kwani nyaraka zote za kusaini mkataba na jinsi alivyochukua pesa zipo.

Mbali na kuchukua pesa hizo Panduka pia ameitia hasara K-Mondo ya zaidi ya sh milioni tatu kutoka na gharama ilizotumia kurekodi nyimbo tatu ambazo sauti yake ipo pamoja na Video hali iliyofanya nyimbo hizo zishindwe kurushwa hewani. Panduka alirekodi wimbo uitwao Kaumia, U Still Mine na Mpenzi Issa huku Video za Kaumia na U Still Mine zikiwa zimetengenezwa.

Comments