MBWANA MATUMLA, MIYEYUSHO WATAMBIANA


PROMOTA WA PAMBANO LA KUWANIA MKANDA UNAOTAMBULOWA NA UBO INTERCONTINETAL , MODY BAWAZIR AKIONYESHA MKANDA HUO KWA WAANDISHI WA HABARI KATIKA HAFLA YA KUTAMBULISHA PAMBANO HILO LITAKALOFANYIKA OKTOBA 30 KWENYE UKUMBI WA DIAMOND JUBILEE, JININI DAR ES SALAAM NA KUWAKUTANISHA MBWANA MATUMLA NA FRANCIS MIYEYUSHO.

MABONDIA wa ngumi za kulipwa nchini Mbwana Matumla na Francis Miyeyusho kila mmoja ametamba kuibuka na ubingwa wa mabara unaotambuliwa na UBO, linalotarajiwa kufanyika Oktoba 30 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.



Pambano hilo la raundi 12 katika uzito wa Bantam limeandaliwa na kampuni ya Dar World Links Limited ya jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na Shirikisho la Masumbwi Nchini (PST).

Wakizungumza na waandishi wa habari leo  kwenye hoteli ya JB Belmont, mabondia hao walisema wapo katika maandalizi makali kwa ajili ya pambani hilo ambapo kila mmoja amejinasibu kumshinda mwenzake.

Matumla ambaye anashikilia mkanda huo, alisema kutokana na maandalizi aliyoyafanya, ana uhakika wa kumshinda mpinzani wake huyo katika raundi ya tano tu, hivyo amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi siku hiyo.
Kwa upande wa Miyeyusho, alisema kuwa hatishiki na uzoefu wa Matumla katika medani hiyo kwani yuko katika mazoezi ya hali ya juu kuhakikisha anamshinda mpinzani wake kati raundi ya nane na kumnyang’anya ubingwa.
Naye mkurugenzi wa Dar Links Limited, Mohammed Bawazir, alisema kuwa mbali na pambano hilo pia kutakuwa na pambano jingine la kuwania ubingwa PST kati ya bingwa mtetezi Juma Fundi na Fadhili Majia watakapokipiga katika uzani wa Fly, raundi kumi.
“Pia kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi ikiwemo lile la Mohammed Rashid Matumla dhidi ya Ramadhan Mashudu (uzito wa Super Bantam), Issa Sewe atazipiga na Ramadhan Shauri, Hassan Kidebe atazipiga na Deo Samwel ambapo mapambano yote haya yatakuwa ya raundi nane,” alisema.
Aidha, Bawazir aliongeza kuwa siku hiyo kutakuwa na pambano jingine litakalowahusisha kinadada ambapo Asha Abubakar ‘Asha Ngedere’ atazichapa na Salma Kiombwa ‘Cheka wa Moro’, pambano litakalokuwa la raundi sita.
Bawazir aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini pambano hilo ambapo mpaka sasa wadhamini waliojitokeza ni pamoja na JB Belmont Hotel, Gazeti la Jambo Leo pamoja na blogu za Michuzi, Mamapipiro na Shafii Dauda.

Comments