MALINZI:NITAONDOA UOZO KWENYE VYAMA VYA MICHEZO

KWA mujibu wa mwenyekiti mpya wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dionis Malinzi, changamoto kubwa ambayo ataifanyia kazi katika uongozi wake ni kuhakikisha anaondoa uozo mwingi uliyo kwenye vyama vya michezo nchini.

Hata hivyo, Malinzi ambaye aliteuliwa juzi na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk.Emmanuel Nchini, kushika nafasi hiyo, alisema ataweka wazi mikakati yake pindi baraza lake litakapozinduliwa rasmi.
Malinzi alisema ili vyama hivyo viweze kufanya kazi kwa mafaniko, kama mwenyekiti anawajibika kuvisimamia kwa ukaribu ili kuondoa uozo uliopo kwenye vyama vyote.
Alisema pindi watakapokabidhiwa rasmi majukumu yao, atakutana na wajumbe wake ili kupanga mikakati ya jinsi gani watakabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya michezo.
Malinzi alisema kuwa migogoro iliyo kwenye vyama hivyo inachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya michezo na hivyo kusababisha kuwa wasindikizaji katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
“Baada ya kukutana na wajumbe wangu, tutakutana na viongozi wote wa vyama ili kufahamiana nao na kuwapa mikakati yetu ya kuimarisha michezo na hivyo baada ya hapo tutaanza kutimiza wajibu wetu,” alisema.
Aliongeza kuwa BMT si mali yake hivyo ameomba wajumbe wa baraza hilo kuwa kitu kimoja katika kutimiza majukumu yao ili kuiletea maendeleo nchi kupitia michezo.

Comments