MAAFANDE WA RUVU SHOOTING WAWACHUKULIA RB WENZAO WA POLISI DOM

UONGOZI wa timu soka ya Ruvu Shooting umewafungulia jarida la mashitaka (RB) wachezaji wa timu ya Polisi Tanzania kutoakana na kumpiga na kumsababishia maumivu dereva wa meneja wa timu yao, Richard Samweli saa chache kabla ya kukwaana juzi kwenye dimba la Jamhuri,mjini Dodoma.
Ofisa habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire, amesema  kwamba wakati wachezaji wakienda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, dereva huyo alikuwa pembeni hivyo kumvamia na kuanza kumshambulia kabla ya viongozi wa Ruvu Shooting kwenda kuamulia.
Alisema baada ya kitendo hicho walikwenda kituo cha Polisi kati mkoani Dodoma na kuomba kibali cha matibabu (PF 3) ili kuweza kupata matibabu na kwenda katika hospitali ya mkoa na baada ya uchunguzi ilibainika kuwa aliumia sehemu za kifua, tumbo na mbavu.
“Baada ya matokeo ya vipimo vya hospitali tulirudi polisi na kufungua jalada namba RB/DOM/9348/2011 kwa wachezaji wa timu hiyo kwa kosa kupigwa na kusababisha maumivu,”Alisema.
Masau alisema kuwa uongozi umesikitishwa na kitendo hicho kisicho cha kiuanamichezo kilichofanywa na wachezaji hao na wameshaandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiomba wachezaji waliohusika kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
“Tumeshawasilisha barua ya malalamiko kwa Mkurugenzi wa mashindano TFF, Sadi Kawemba kupinga suala la timu mwenyeji kumfanyia mgeni vurugu hivyo tunaamini watachukua hatua zinazostahili.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara timu hizo zilitoka suluhu ya bila kufungana.

Comments