KUMEKUCHA AIRTEL RISING STARS

HATUA ya pili ya mashindano ya kusaka nyota wa soka wenye umri chini ya miaka 17 ‘Airtel Rising Stars’ inatarajiwa kuanza kufanyika jumamosi kwenye uwanja wa Karume ambapo kombaini ya mkoa wa Mwanza itakipiga na kombaini ya Morogoro.


Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Septemba 18 Iringa itakipiga Dar es Salaam, wakati Septemba 19 itakuwa mapumziko, kabla ya Septemba 20 Moro kukwaana na Iringa huku Dar es Salaam ikicheza na Mwanza.

meneja uhusiano wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Jackson Mmbando alisema kwamba timu shiriki zinatarajiwa kuanza kuwasili ijumaa na zitaweka kambi katika Shule za Filbert Bayi zilizopo Kibaha, jijini Dar es Salaam.

Alisema kupitia hatua hiyo ndipo watasakwa nyota sita toka katika timu shiriki ambao wataungana na wengine kutoka nchi za Afrika zinazotumia mtandao wa Airtel na kuingia katika kambi maaum itakayofanyika nchini kuanzia Oktoba 27 hadi Novemba 3.

“Kila nchi shiriki itatoa vijana sita ambapo kliniki hii itaendeshwa na wakufunzi kutoka klabu ya soka ya Manchester United ya Uingereza wakishirikiana na wa hapa, hivyo naamini vijana watakaobahati kuweko katika kliniki hiyo watapata faina kubwa sana,”Alisema Mmbando.

Mpango huo ambao kwa hapa nchini ulizinduliwa na nyota wa zamani wa Manchester United , Andy Cole ulianza kwa kuhusisha timu 24 kutoka shule za mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Iringa na Morogoro ambapo baada ya kumalizika kwa hatua ya kwanza,hivyo kila mkoa kuunda timu.

Comments