KILIMANJARO BEER FESTIVAL KURINDIMA VIWANJA VYA LEADERS OKTOBA MOSI


TAMASHA kubwa la kwanza la Bia Tanzania lenye lengo la kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania na kuwaleta Watanzania pamoja, linatarajiwa kufanyika Oktoba mosi na mbili katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, aliwaambia waandishi wa habari  kwamba tamasha hilo la aina yake litakalojulikana kama ‘Kilimanjaro Beer Festival’ litaambatana na burudani pamoja na michezo mbalimbali.
Alisema Watanzania hawana budi kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo ili kupata fursa ya kusherehekea, kuburudika na kubadilishana mawazo na wadau kutoka tasnia tofauti.
“Kutakuwa na burudani kutoka katika bendi tofauti, wasanii wa ndani na nje ya nchi, michezo mbalimbali, vyakula, vinywaji na zawadi za kila aina, yote hiyo ni katika kujivunia mafanikio yetu Watanzania baada ya miaka 50 ya Uhuru,” alisema.
Kavishe aliongeza kwamba tamasha hilo ambalo llimeandaliwa na Bia ya Kilimanjaro kwa kushirikiana na Kampuni ya Bongo 5, Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa na taasisi ya Goethe, litaanza saa nne asubuhi hadi saa mbili usiku.
“Kutakuwa na ulinzi wa kutosha siku hiyo ambapo kiingilio kitakuwa sh 10,000 kwa siku zote mbili na shilingi 7,000 kwa siku moja,” alisema.

Comments