K-MONDO SOUND WAMRITHI JD&MACHOZI BAND ZHONG HUA GARDEN

MWANAMUZIKI wa muziki wa kizazi kipya akiimba miondoko ya Zouk, Vumilia Abrahm akiwa na bendi yake ya K-Mondo Sound wameingia mkataba wa kutumbuiza katika ukumbi wa Zhong Hua Garden uliopo Victoria mkabala na benki ya Barclays.

Vumilia ambaye kwa sasa anatamba kibao chake Nasepa amechukua nafasi iliyoachwa wazi na nguli wa muziki wa kizazi kipya, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ ambaye alikuwa akitumbuiza hapo kila Jumamosi. Tangu kuondoka kwa Jaydee Jumamosi palikuwa pakipigwa disko.
K-Mondo Sound ambayo inaongozwa na Teacher Richard Mangustino imemuongeza pia katika kikosi hicho mwanamuziki mwingine aliyewahi kutamba na kibao cha Dokta, Salum Kumpeneka katika safu yake ya uimbaji.
Akizungumzia kufanya kwao onyesho, Zhong Hua Garden, Vumilia alisema ni uamuzi wa kuwasogezea zaidi mashabiki wao burudani baada ya kupiga maeneo ya mbezi kwa muda mrefu zaidi.
“Mashabiki waliokuwa wakilalamika kuwa Mbezi mbali sasa wataweza kupata uhondo wa nyimbo zetu, kama inavyojulikana bendi yetu inapiga muziki wa aina zote, hivyo ni bora waje kushuhudia makali yetu, shoo itakuwa maalum, na zitapigwa zote kali kutoka K-Mondo pamoja na copy za nje,” alisema.
Naye Mangustino alisema K-Mondo ni taratibu haina haraka na imekuja kuonyesha wapenzi wa burudani nini maana ya burudani. Amesema bendi yao bado itaendelea kutumbuiza Triz Motel kwa siku za Ijumaa na Jumapili itakuwa Giraffe Hotel.
Mbali na sehemu hizo, Mangustino amesema wakazi wa Oysterbay wakae mkao wa kula kwani muda si mrefu kila siku ya Jumatano burudani ya K-Mondo Sound itawasogelea kwao.
K-Mondo sasa inatamba na nyimbo zake za Njiwa, Magambo, Nelly, Nasepa, Tatizo Umasikini, Utanikumbuka, Sheria na nyingine nyingi.

Comments