HASSANOO APANDISHWA KIZIMBANI



MWENYEKITI wa Chama cha soka Mkoa wa Pwani (COREFA) Hassan Othman ‘Hassanoo’ na wenzake watatu, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na shitaka la kula njama na kuiba tani 26 za shaba zenye thamani ya Shilingi mil. 400 mali ya Kampuni ya Liberty Express Ltd ya Dar es Salaam.
Mawakili wa Serikali Andrew Rugarabamu na Aneth Kaganda,walidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Devotha Kissoka kuwa Agosti 26, mwaka huu maeneo ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, washitakiwa walikula njama na kuiba mali hiyo kwenye gari namba T 821 BCL iliyokuwa inasafirishwa kwenda Zambia.
Wakili Rugarabamu alidai katika kosa la nne, washitakiwa hao wanadaiwa kupokea tani hizo za shaba kinyume cha sheria huku wakijua wazi mali hiyo iliibwa.
Baada ya kusomewa mashitaka yao, Wakili Kaganda aliiomba Mahakama kama itaona umuhimu wa kuwapa washitakiwa hao dhamana kwa kuzingaria sheria ya mwenendo wa kesi za jinai namba 148 kifungu kidogo (e) sambamba na masharti ya kuwa na wadhamini wa kuaminika.
Hakimu Kissoka alisema dhamana kwa washitakiwa hao iko wazi kwa sababu makosa yao yanadhaminika kwa mujibu wa sheria, ambapo aliwataka kuwa na Shilingi mil. 50, na wakishindwa, watoe kitu kingine chenye thamani ya fedha hizo.
Aidha, washtakiwa hao, wanapaswa kuwa na mdhamini mmoja ambaye ataithibitishia Mahakama kama yupo tayari kumdhamini kwa kiasi cha sh milioni 20.
Upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Majura Magafu ulipinga hoja iliyotolewa na wakili wa serikali kuwa haina msingi, kwani kifungu hicho alichotumia hakitoi mwanya kwa upande wa mashitaka kuhakiki nyaraka zinazotolewa mahakamani.
Hata hivyo, Hassanoo alipata dhamana, huku watuhumiwa wengine Wambura Kisiroti (32), Najim Msenga (50) na Salim Shekibula (29)wakirudishwa Mahabusu hadi Jumatatu ambapo shauri hilo itatajwa tena.

Comments