AIRTEL RISING STARS:MOROGORO YAIBUGIZA IRINGA 8-0

Mzamir Yassin  wa timu ya kombaini ya Mkoa wa Morogoro, akimtoka Anwar Kihaga wa Iringa baada ya kumlamba chenga michuano ya kukuza vipaji vya soka kwa vijana ya Airtel Rising Stars, jana kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Morogoro iliibugiza Iringa mabao 8-0.

Michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 iliendelea hapo siku ya Jumanne ambapo timu ya Morogoro iliishushia kipigo cha 8-0 timu ya Iringa katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume Jijini Dar es Salaam. Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa timu ya Iringa kupoteza kwa idadi kubwa ya magoli kwani kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa siku ya Jumapili ilishuhudia ikipata kipigo cha aibu cha magoli 10-0 kutoka kwa timu ya Dar es Salaam.
Michuano hiyo ambayo imedhaniwa na Kampuni ya Airtel na ambayo iko kwenye ngazi ya Taifa, ina lengo ya kupata vijana bora sita ambao watajiunga na wenzao kutoka Kenya, Malawi, Uganda na Sierra Leon katika kambi maalum ya Kimataifa ya mpira wa soka ambayo itafanyika hapa Jijini Dar es Salaam mnamo mwishoni mwa mwezi wa Octoba mwaka chini ya uangalizi wa waalimu wa soka kutoka Klabu ya Manchester United ya Uingereza.
Katika mchezo huo wa Jumanne, timu zote ziliuanza mchezo kwa kasi huku kila timu ikionyesha tahadhari kubwa kuepuka kufungwa goli la mapema lakini kadri muda ulipokuwa unakwenda, Iringa walionekana kupoteza kasi ya mchezo na katika dakika ya 18, Ibrahim Hussein ailiiandikia timu yake bao la kwanza baada ya mabeki wa Iringa kumuachia wakidhani ameotea. Kuingia kwa bao kulifanya Morogoro kuongeza mashambulizi na dakika ya 27 Kassim Jungu akaongeza bao la pili. Dakika mbili baadae, Ibrahim Hussein aliongeza la tatu na hadi timu zinakwenda mapumziko, mabao yalikuwa ni matatu kwa bila.
Kwenye kipindi cha pili, Morogoro waliendeleza kasi ile na mnamo katika dakika ya 51 na 53 ya mchezo, Graham Naftali aliongezea timu yake bao la nne na tano. Huku Iringa wakionekana kupoteana kabisa, walijikuta wakiongezwa bao la sita katika dakika ya 72 mfungaji akiwa ni Graham Naftali tena. Goli la saba na nane yalifungwa na Ibrahim Hussein na Joseph Mbawa katika dakika ya 80 na 89.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena hapo Jumatano kwa timu ya Dar es Salaam kucheza na timu ya Mkoa wa Mwanza.

Comments