WASANII WAASWA KUTOUZA HAKIMILIKI ZAO

 Mshauri wa masuala ya Biashara na Mjasiriamali Bw.Alitenus Millinga (Katikati) akiongea na wasanii kuhusu masuala mbalimbali ya kuboresha masoko ya kazi zao kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.Kulia ni Kaimu Mratibu wa Jukwaa Bw.Alistide Kwizela na Mwenyekiti wa program,Bw.Godfrey L. Mngereza
Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA,Bw.Godfrey L. Mngereza akisisitiza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.Alisisitiza kwamba,BASATA itaendelea kuwakutanisha wasanii na wataalam mbalimbali kwalengo la kuwapatia wasanii na waandishi wa ahabari ufahamu wa tasnia ya sanaa na utamaduni.

Na Mwandishi Wetu

Wasanii nchini wametakiwa kuacha tabia ya kuuza hakimiliki ya kazi wanazobuni kwani kwa kufanya hivyo wanapoteza haki ya umiliki wa kazi zao kwa miaka yote ya maisha yao na miaka hamsini baada ya kifo.
Akizungumza wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu katika Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Mshauri wa masuala ya biashara na mjasiriamali Bw.Alitenus Millinga alisema kwamba, kumekuwa na taarifa za wasanii kuuza haki ya umiliki wa kazi za ubunifu kutokana na kusaka fedha za haraka pasi na kuzingatia athari zake.
“Uthamani wa kazi ya ubunifu huanza na msanii kumiliki haki za ubunifu.Tatizo la wasanii wetu wamekuwa hawathamini hakimiliki na wamekuwa wakiuza bila kuangalia kesho.Wanaangalia leo-leo tu.Hii ni changamoto kubwa” alisema Bw.Millinga.
Aliongeza kwamba,haki za msanii kumiliki ubunifu wake kwa mujibu wa sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki hudumu kwa miaka yote ya uhai wa msanii na miaka 50 baada ya kifo chake hivyo hulka yoyote ya wasanii kuuza hakimiliki kwa kutazama leo tu inawakosesha haki na mapato mengi.
Hata hivyo,alikosoa vikali tabia ya baadhi ya wasanii kunakili kazi za wengine hali inayoifanya tasnia ya sanaa nchini ikose utambulisho wa Taifa letu na kuzifanya kazi hizo sishuke thamani na kudumu kwa muda mfupi.
“Wasanii ndiyo msingi wa ubunifu na ubunifu ni chanzo cha kutatua matatizo na kuleta mambo mapya.Tukiwa na wasanii wa kunakili kila kitu basi maana yake hata taifa lenyewe linakosa utambulisho pia ubunifu” alisisitiza Millinga.
Alizidi kueleza kwamba,ili msanii aweze kufaidi kazi za sanaa lazima azingatie thamani ya ubunifu wake ikiwa ni pamoja na kuzalisha kazi zenye ubora na kulenga soko,kuzingatia mikataba ya masoko,kupanga bei zenye kuzingatia wanunuzi na kuzisambaza kikamilifu.
Aliyataja masuala kama uuzaji wa hakimiliki, kutozingatia mikataba,uharamia na kupanga bei pasipokuzingatia hali ya uchumi kama changamoto zinazowakabili wasanii katika kupata mafanikio ya kazi zao.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Sanaa, Bw.Godfrey L. Mngereza alisema kwamba,somo lililotolewa na Bw.Millinga kwa wasanii ni kubwa sana na wanapaswa kulifanyia kazi ili kuweza kupiga hatua.

Comments