VODACOM YAKABIDHI VIFAA KWA TIMU ZITAKAZOSHIRIKI LIGI KUU SOKA TANZANIA BARA

MKUU WA UDHAMINI WA VODACOM GEORGE RWEHUMBIZA KULIA AKIKABIDHI VIATU NA JEZI WATAKAOTUMIA WAAMUZI WA LIGI HIYO KWA MAKAMU WA KWAZANZA WA RAIS WA TFF ATHUMAN NYAMLAN, KULIA NI MKURUGENZI WA MASHINDANO WA TFF, SADI KAWEMBA
KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania  imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu 12 zitakazoshiriki ligi kuu soka Tanzania Bara msimu wa 2011/2012 inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwenye hoteli ya Kilimanjaro, mkuu wa udhamini wa Vodacom George Rwehumbiza alisema vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi mil.352 ni sehemu ya udhamini wao katika ligi hiyo.
Alisema ili kuhakikisha wanaboresha udhamini wao, kabla ya kutoa vifaa hivyo walikutana na vilabu husika pamoja na Shirikisho la soka Tanzania (TFF) ili kujadiliana ubora wa vifaa unavyostahili.
Rwehumbiza aliongeza kuwa mbali na kuzipatia timu vifaa hivyo , pia wametoa vifaa kwa waamuzi watakaochezesha ligi hiyo.
Vifaa hivyo ni pamoja na seti 60 za jezi na mipira 60 kwa kila timu, viatu, soksi, vilinda ugoko, mabegi ya safari na mipira ya jabulani kwa waamuzi.
Naye makamu wa kwanza wa TFF Athuman Nyamlani, pamoja na kuishukuru Vodacom kwa udhamini huo ambao kwa kiasi kikubwa umeboreshwa alitoa wito kampuni hiyo kuvisaidia vilabu visivyojiweza.
Akizungumza kwa niaba ya vilabu vitakavyoshiriki ligi hiyo, meneja wa timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro Abdul Masamaki, pamoja na kuishukuru Vodacom aliiomba kuvidhamini vilabu visivyojiweza kwa asilimia 100.
Alisema,iwapo Vodacom itazidhamini timu hizo kwa asilimia 100 itasaidia kuleta ushindani katika ligi hiyo kuanzia mwanzo mpaka mwisho na hivyo kufanya bingwa aweze kuwakilisha vema kwenye michuano ya kimataifa.
Timu zitakazoshiriki ligi hiyo ni pamoja na African Lyon, Azam FC, Coastal Union, JKT Ruvu, Moro United, JKT Oljoro, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Simba SC, Toto African, Polisi Tanzania, Ruvu Shooting na Yanga ambao ni mabingwa wateytezi wa ligi hiyo.

Comments