VOCTOR COSTA AMLILIA BOBAN STARS


SIKU moja baada ya kutangazwa kwa kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, beki wa kati wa Simba, Victor Costa aliyeitwa kwenye timu hiyo amesema kocha wa timu hiyo, Mdenmark Jan Poulsen amekosea kutomuita kiungo, Haruna Moshi ‘Boban’.
Costa aliyerejea Simba msimu huu akitokea Msimbiji alikokuwa akicheza soka ya kulipwa, alisema kwamba sababu zilizotolewa na Poulsen kuhusu kumuacha kwake Boban kwamba hana uwezo wa kucheza dakika 90, hazina msingi.
“Nimesikia kocha amesema Boban hawezi kuichezea Stars, kwa sababu ana uwezo wa kucheza dakika 25 tu ndani ya dimba, hii si sahihi kwani kuna wachezaji wengine wameitwa kwenye kikosi hawawezi kucheza hata muda alioodai wa Boban,” alisema na kuongeza.
“Humo humo kuna wachezaji wanaweza kucheza dakika tano tu, 10, 20 na hata wengine wanaishia mazoezini tu, sasa kwa kiwango alichonacho Haruna kwa sasa, nadhani angeisaidia sana Stars,”alisema.
Poulsen juzi alitaja wachezaji 23 wa kuunda Stars itakayoingia kambini kesho kujiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani, dhidi ya Algeria, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Septemba 3, mwaka huu.
Hao ni makipa; Shaaban Dihile (JKT Ruvu Stars), Juma Kaseja (Simba) na Shaaban Kado (Yanga); mabeki wa pembeni ni Nahodha Shadrack Nsajigwa (Yanga), Idrisa Rajab (Sofapaka, Kenya) na Amir Maftah (Simba), wakati mbali na Costa mabeki wengine wa kati ni Aggrey Morris (Azam) na Juma Nyosso  wa Simba pia.
Viungo wakabaji ni Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Nurdin Bakari (Yanga), Shaabani Nditi (Mtibwa Sugar), Juma Seif (Yanga) na Jabir Aziz (Azam), wakati viungo wachezeshaji ni Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), Mrisho Ngassa (Azam) na Salum Machaku (Simba) wakati washambuliaji ni Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Mbwana Samatta (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Ramadhani Chombo (Azam), Danny Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Athumani Machuppa (Vasalund IF, Sweden) na John Bocco (Azam).
Baada ya kutaja kikosi huku akiwaacha wachezaji wawili vipenzi vya wapenzi wa soka nchini beki Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ wa Yanga na kiungo wa Simba, Boban, Poulsen alisema; “Boban hana sifa za kuchezea timu ya taifa, hawezi kuhimili kucheza muda mrefu, nilimuona katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, alicheza kwa dakika 25 tu, muda mwingine alikuwa akizunguka tu uwanjani. Cannavaro anaumwa,” .

Comments