UEFA KUMCHUNGUZA WENGER


Arsene Wenger huenda akakabiliwa na hatua zaidi za nidhamu kutoka Uefa baada ya kuthibitishwa mawasiliano yake na benchi la ufundi la Arsenal yanachunguzwa. Wenger alikuwa akitumikia adhabu ya kutokaa kwenye benchi la timu hiyo wakati wa mechi ya kufuzu kwa Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Udinese.
Arsenal ilikuwa inahisi Wenger huenda angeruhusiwa kupitisha ujumbe kwa msaidizi wake Pat Rice kwa kupitia kocha wa kikosi cha kwanza Boro Primorac. Lakini Wenger alionywa wakati wa kipindi cha mapumziko kwamba hilo haliruhusiwi.
Uefa imethibitisha kwa BBC kwamba wanachunguza kama kulikuwa na uvunjaji wa kanuni.
Arsene Wenger alionekana akikaa karibu na Primorac na hakuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari baada ya mechi, akisisitiza kuzuiwa kwake kukaa kwenye benchi la ufundi pia kunamzuia kufanya shughuli na wanahabari.
Maafisa wa Arsenal wameshangazwa na msimamo huo wa Uefa, huku ikifahamika wakati wa mkutano kabla ya mechi kwamba Wenger angeweza kutuma ujumbe kwa jopo la makocha kupitia mtu wa tatu ambaye ni Primorac.
Wenger kwa sasa hana budi kusubiri iwapo Uefa wataona mawasiliano yake na Rice kama ni uvunjaji wa taratibu na achukuliwe hatua, ingawa wanaweza kukubali hiyo inaweza kuwa ni matokeo ya kutoelewa kuliko kwenda kinyume na kufungiwa kwake kukaa katika benchi la ufundi.
Meneja huyo wa Arsenal kukatishwa tamaa kwake kunaonekana kumeongezeka baada ya timu yake kushindwa kufunga mabao zaidi baada ya kupata bao moja lililofungwa na Theo Walcott.
Mara nyingi Udinese walionekana wakiisumbua Arsenal, lakini winga wa England Walcott amesisitiza Arsenal walikuwa katika "nafasi nzuri" na wanakusudia kufanya vizuri zaidi baada ya kuondokewa na nahodha wao Cesc Fabregas wiki hii.
Walinzi wa Arsenal Kieran Gibbs na Johan Djourou waliumia msuli wa paja wakati wa mechi hiyo.
Kwa sasa kuna wasiwasi iwapo wataweza kucheza mwishoni mwa wiki dhidi ya Liverpool, huku Jack Wilshere naye akiwa hajapona sawasawa kutokana na kuumia kifundo cha mguu.

Comments