TWIGA STARS WAITEGA TFF


WAKATI mechi mbili za kirafiki za timu ya taifa ya soka ‘Taifa Stars’ zimeyeyuka, timu ya wanawake ‘Twiga Stars’ nayo ipo shakani kucheza mechi za kirafiki walizopanga.

Twiga Stars imepanga kucheza mechi za kirafiki kwa lengo la kujifua kwa ajili ya Michezo ya Afrika ‘All Africa Games 2011’ itakayofanyika Maputo, Msumbiji mwezi ujao.
Kocha mkuu wa Twiga Stars, Charles Mkwasa alisema Dar es Salaam jana wachezaji wote wameripoti kambini Msimbazi Centre, Dar es Salaam kwa ajili ya mechi za majaribio wakisubiri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mkwasa alipendekeza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Kenya na Uganda ambazo alisema itakuwa ni muafaka kupima viwango vya vijana wake kabla ya michuano hiyo ya bara la Afrika.
Mapendekezo ya Mkwasa kwa ajili ya mechi za kirafiki ilikuwa ni kuwa na mashindano madogo ya timu tatu. Twiga Stars walipita moja kwa moja kwenye Michezo ya Afrika baada ya wapinzani wao Sudan kujitoa.
Twiga Stars pia walipita bila upinzani dhidi ya Uganda na Kenya. Watashiriki michezo hiyo kwa mara ya kwanza.
“Tunasubiri majibu ya TFF kuhusiana na mechi tulizopendekeza, vijana wanajituma mno mazoezini.
“Kwa kuzingatia kwamba wamepita kwenye michuano bila ya upinzani, tunahitaji mashindano ya majaribio kujiweka fiti kwa mashindano,” alisema Mkwasa.
Leo wachezaji wa Twiga Stars watafanyiwa uchunguzi wa afya Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na baadaye wataendelea na mazoezi Ufukwe wa Coco.
Twiga Stars wataanza kampeni za All Africa Games dhidi ya 'Black Princesses' wa Ghana Septemba 5 Maputo. Twiga Stars wapo Kundi B pamoja na Afrikia Kusini, Zimbabwe na Ghana.
Mechi ya pili nitakuwa Septemba 8 dhidi ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ na Twiga Stars watamaliza mechi ya makundi na Zimbabwe siku tatu baadaye.
Mkwasa alisema ana matumaini timu itafanya vema Maputo. Twiga Stars waliweka historia mwaka jana walipofuzu fainali za Afrika kwa wanawake zilizofanyika Afrika Kusini.

Comments