TWIGA STARS NAYO KAMBINI

TIMU ya Taifa ya Wanawake 'Twiga Stars' inaingia kambini leo kwa maandalizi yake ya michuano ya Michezo ya Afrika 'All Afrika Games' itakayofanyika mjini Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3 hadi 18.

Kocha Boniface Mkwasa alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa anafahamu muda uliobaki ni mfupi isipokuwa atahakikisha programu aliyoiandaa inamalizika kabla ya fainali hizo.
"Timu imeanza mazoezi (leo) jana kwa ajili ya ushiriki wake Michezo ya Afrika kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, tutakuwa tukifanya mazoezi hayo asubuhi na jioni," alisema Mkwasa.
Alisema ataanza na programu ya kutafuta stamina na kasi ya mchezo kwa kufanya mazoezi ya kuzunguka uwanja kwa kukimbia na gym kwa ajili ya kutafuta stamini na nguvu kwa wachezaji hao.
Hata hivyo; Shirikisho la soka limesema liwagharamia watu wanne kwenda Msumbiji kutokana na serikali kusema itawagharamia watu 20 tu kwenye msafara huo.
"Serikali imesema itagharamia watu 20 tu watakaoenda Msumbiji, lakini TFF tutagharamia watu wanne ili kufika idadi ya msafara wa watu 24 watakaoenda Maputo," alisema Wambura.
Alisema timu hiyo itakabidhiwa leo kwenye Kamati ya Olimpiki Tanzania 'TOC' kwa ajili ya kuanza kambi rasmi ambapo itakuwa chini ya uangalizi wa kamati hiyo mpaka pale itakapoondoka kwenda kushiriki michezo hiyo.
Twiga Stars imepangwa kundi B katika michuano hiyo pamoja na Afrika Kusini 'Banyana Banyana', Ghana na Zimbabwe 'Mighty Worriors'.

Comments