TIMBE AFICHUA SIRI YA VIPIGO SUDAN


KOCHA wa Yanga, Sam Timbe raia wa Uganda, amesema kwamba kufungwa mechi zote mbili na El Hilal ya Sudan katika ziara yao kujiandaa na msimu mpya nchini Sudan, kulitokana na uzoefu mdogo wa wachezaji wake. "Tumejifunza mengi kutoka kwenye mechi mbili dhidi ya Al Hilal, lakini kilichosababisha kufungwa kwa vijana wangu ni kukosa uzoefu pamoja na uchovu.
‘’Kiufundi timu iko vizuri na hii ziara tuliyoipata tumejifunza mambo mengi kiufundi na kugundua mapungufu ya wachezaji wangu,’’alisema Timbe kocha aliyetwaa makombe ya Kagame mara nne akiwa na timu za Villa na Polisi ya Uganda, Atraco ya Rwanda na Yanga anayoifundisha sasa.
‘’Wachezaji wangu nimegundua hawana uzoefu wa kutosha na wanachoka mapema, hii ni kutokana na aina ya mabao tuliyofungwa, tatizo ambalo nitalifanyia kazi katika mazoezi ya siku zilizobaki kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu,’’alisema Timbe.
Aliongeza kuwa," mechi zote mbili tulianza kufunga, lakini baada ya hapo wanatoa mwanya kwa wapinzani kusawazisha na kuwapa nafasi ya kufunga mabao mengine ya ushindi.
Katika mchezo wa pili waliocheza juzi Jumatano Yanga ilifungwa tena mabao 3-1, bao lao Yanga likifungwa na Mghana Kenneth Asamoah, katika mchezo wa kwanza uliofanyika Agosti 6, Hamisi Kiiza alifuga goli la kufutia machozi la Yanga ilipofungwa na Al Hilal inayofundishwa na Micho aliyewahi kuinoa timu hiyo ya mtaa wa Jangwani na Twiga.
Yanga iliwasili jana saa 7:30 mchana, wakitokea Sudan walipokuwa na ziara ya mechi ya mechi za kirafiki kutokana na mwaliko wa Al Hilal.



Comments