TFF: TUTAIFUNGIA SIMBA IKIGOMEA MECHI


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema litatumia sheria za Fifa kuiadhibu Simba kama wakigomea kuingiza timu uwanjani kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii hapo kesho. Sheria hiyo ya Fifa itatumika endapo Simba watagoma kuingia uwanjani siku ya mchezo na watafungiwa au kutozwa faini kwa kitendo hicho ambacho sio cha kimchezo. Uamuzi huo wa TFF umekuja baada ya viongozi wa Simba kung'ang'ania na kugoma kuingiza timu uwanjani kama mshambuliaji wake kutoka Jamhuri Afrika ya Kati, Gervais Kago hataruhusiwa kucheza.
Mwenyekiti wa klabu ya hiyo, Ismail Aden Rage alisema kuwa mazingira ambayo Kago amezuiliwa kushiriki katika mechi hiyo ya Ngao ya Jamii na Ligi ni hujuma kwani Yanga ilimtumia Kenneth Asamoah mwaka jana katika mechi kama hiyo na TFF haikuwahi kumzuia kama inavyofanya hivi sasa.
Rage alisema kuwa hati ya Uhamisho ya Kimataifa ya Kago ilifika nchini tangu Julai 16 mwaka huu na mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya kimaandishi kutoka TFF ikimzuia au kuzungumzia matatizo ya uhamisho wake.
“Hapa kuna hujuma, sisi ni washirika wa TFF na kuna njia za mawasiliano, sio Mgongolwa (Alex) na kamati yake wala TFF watendaji ambao wametuandikia kutujulisha suala hili, sisi hatuna haja ya kuwapa wao taarifa za kimaandishi kama tutagomea, kupitia gazeti lako, ndiyo tunatoa taarifa hiyo,” alisema Rage.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema jijini Dar er es Salaam jana kuwa kanuni za uhamisho kwa wachezaji wa kulipwa ndizo zilizomzuia Kago na sio uamuzi wa kiongozi mmoja kama ambavyo viongozi wa Simba wamekuwa wakielekeza shutuma kwa mkurugenzi wa mashindano wa shirikisho hilo, Sad Kawemba.
"Ni jambo linalosikitisha kuona viongozi wa Simba wanakwepa kuwajibika na kuishia kuelekeza shutuma kwa kumtaja kiongozi wa TFF, kama wana hoja wawasilishe kwetu na sisi tutawaelekeza, huu utaratibu wa kuongea hovyo hovyo sio mzuri, mbaya zaidi wanamtaja Sad kwamba ndio anawawekea mizengwe,waelewe kwamba wanahatarisha maisha ya mtu,hauwezi kujua mashabiki wanapokeaje.
"Kanuni ndizo zilizomzuia Kago na sio suala la kiongozi mmoja wa TFF, Sad peke yake hawezi kuwa na mamlaka ya kumzuia mchezaji asicheze, mkataba wa usajili wa Kago na Simba unasema atasajiliwa kama mchezaji wa kulipwa, lakini utaratibu waliotumia kumwamisha ni wa ridhaa, hapo ndipo tatizo lilipo.
"Kwa mantiki hiyo hakuna njia nyingine ya kufanya wakati huu kwa sababu muda wa usajili umepita, zaidi ya hapo Simba wanatakiwa kusubiri hadi wakati wa kipindi cha dirisha dogo la usajili ili waweze kumsajili kwa utaratibu unaotakiwa yaani TMS," alisema Osiah.
Utaratibu huo wa TMS ambao ni (Transfer Match System-TMS) ni mfumo mpya wa Uhamisho ambao unadhibiti uhamisho wa Kimataifa wa Wachezaji na kuondoa kasoro nyingi zikiwemo zile za Wachezaji kumilikiwa na Kampuni badala ya Klabu wanazochezea na ununuzi wa Wachezaji hao unaohusishwa na kuhodhi fedha kinyume cha sheria, ambao klabu zote za Ligi Kuu tayari zina namba zao maalumu za kuingia (passwords).
Wakati TFF ikimzuia Kago tayari ilishabariki uhamisho wa aina hiyo kwa wachezaji wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2011/2012.
Wachezaji ambao maombi yao ya uhamisho yaliwasilishwa TFF kwa njia ya barua ni Shabani Kado kutoka Mtibwa Sugar kwenda Yanga, Salum Machaku kutoka Mtibwa Sugar kwenda Simba na Idrisa Rajab kutoka African Lyon kwenda Yanga.
Mwanzoni mwa mwaka huu wakati FIFA ilipoutambulisha mfumo huo mpya wa Uhamisho ilisema njia hiyo mpya itadhibiti uhamisho wa Kimataifa wa Wachezaji na kuondoa kasoro nyingi zikiwemo zile za wachezaji kumilikiwa na Kampuni badala ya klabu wanazochezea na ununuzi wa wachezaji hao unaohusishwa kuhodhi fedha kinyume cha sheria.
Katika mfumo wa TMS uanaotumia mtandao, ili kukamilisha uhamisho wa mchezaji inabidi klabu zinazouza na kununua mchezaji ziingize kwenye mtandao taarifa zote zinazotakiwa kuhusiana na mchezaji anaehamishwa zikiwemo ada ya uhamisho, mshahara wa mchezaji huyo, Wakala wake au Mwanasheria wake na muda wa mkataba wake, Pia, ada ya uhamisho ni lazima itoke Benki moja kwenda nyingine.
Akiuzungumzia mfumo huo,Meneja Mkuu wa TMS, Mark Goddard alisema: “Huu ni mradi mkubwa wa FIFA. Haujabadilisha sheria za uhamisho bali unadhibiti uhamisho na kuondoa kasoro na dosari nyingi.”
Kwa mujibu wa kanuni za TFF zilizopo hivi sasa kwa sababu shirikisho hilo halijatoa kanuni mpya, kanuni ya 33 inayozungumzia hadhi za wachezaji wa ridhaa na wachezaji wa kulipwa inasema (1) Wachezaji wanaoshiriki katika Soka Rasmi ni wa Ridhaa au wa kulipwa.
(2 Mchezaji wa Kulipwa ni mchezaji mwenye mkataba wa maandishi na Klabu na analipwa zaidi ya gharama halisi anazoingia kutokana na shughuli zake za soka. Wachezaji wengine wote wanahesabiwa kuwa ni wa Ridhaa.
Hata hivyo upo umuhimu wa kuwa na kanuni mpya ambazo zitaelezea kazi za mchezaji wa ridhaa na mchezaji wa kulipwa

Comments