TASWA YAPONGEZA TIMU YA GOFU WA NAWAKE KLWA KUTWAA UBINGWA WA AFRIKA MASHARIKI NA KATI


CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinatoa pongezi kwa timu ya Taifa ya gofu ya wanawake ya Tanzania ‘Tanzanite Stars’ ilitwaa ubingwa wa mashindano ya gofu ya Kombe la Challenge kwa wanawake katika nchi za Afrika Mashariki na Kati. Mashindano hayo yalianza Agosti 16 hadi Agosti 18, mwaka huu kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dar es Salaam.
TASWA imekunwa na mafanikio hayo na inatoa pongezi za dhati kwa timu hiyo kuweza kutetea ubingwa wake katika mashindano ambayo yanafanyika kila baada ya miaka miwili ambpo yalikuwa ya pili na ya viwanja 54.
Tunasema vijana wetu wanastahili pongezi kwani nchi zote nne kutoka zilizoshiriki ambazo ni Kenya, Uganda, Zambia na wenyeji Tanzania zipo juu katika mchezo huo kwa wanawake.
Nchi za Rwanda, Burundi, Malawi, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) zilishindwa kushiriki, lakini tatizo kubwa ni kukosa timu za wanawake.
Tanzania ambao walikuwa mabingwa watetezi wa Kombe hilo ambalo kwa mara ya kwanza walitwaa mwaka 2009 Kampala, Uganda walitetea vema kwa kutwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Hayo ni mafanikio makubwa katika uongozi mpya wa Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) chini ya Rais, Mbonile Burton tangu kuingia madarakani Juni mwaka jana. Mafanikio haya yanafuatia yale ya kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Afrika ya gofu kwa wanawake Abuja, Nigeria mwaka jana.
Pia TLGU imeweza kutangaza vema gofu ya wanawake na kuweka historia ya kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa kwa mara ya kwanza.
Mwaka huu Tanzania wameibuka mabingwa kwa kishindo zaidi wakiwaacha wapinzani wao Zambia walioshika nafasi ya pili kwa tofauti ya mikwaju (strokes) 31. Mwaka 2009 ugenini walishinda kwa tofauti ya mikwaju 20.
Tunaomba wachezaji wa Tanzanite Stars wakiongozwa na nahodha Madina Iddi, Ayne Magombe, Angel Eaton na Hawa Wanyeche waone mafanikio haya waliyoyapata Watanzania wote tunayajali.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
22/08/2011

Comments