SUAREEEEEEEZ KUDADADAAADEEKI... ARSENAL PWA!


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez jana aliiwezesha Liverpool kupata ushindi wa kwanza mbele ya Arsenal FC katika Ligi Kuu ya England tangu mwaka 2000, kwenye Uwanja wa Emirates.
Bao la kujifunga la Aaron Ramsey dakika ya 78 liliwapa Wekundu wa Anfield bao la kuongoza, wakati Ignasi Miquel alipopiga mpira kuondosha hatarini, lakini ukamgonga mwenzake huyo na kutinga nyavuni.
Wakati huo, tayari Arsenal ilikuwa imekwishampoteza mchezaji mmoja wakati Emmanuel Frimpong alipoonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu Lucas.
Mchezaji aliyeingia uwanjani akitokea benchi, Suarez alifunga bao la pili dakika ya 90, baada ya kuiwahi pasi ya kuchomekewa na Raul Meireles.
Katika mchezo huo, kikosi cha Liverpool kilikuwa; Reina, Jose Enrique, Agger, Carragher, Kelly, Henderson, Downing, Lucas, Adam, Carroll/Suarez dk 71 na Kuyt/Meireles dk 71.
Arsenal; Szczesny, Sagna, Vermaelen, Koscielny/Miquel dk 15, Jenkinson, Nasri, Walcott/Bendtner dk 80, Ramsey, Arshavin/Lansbury dk 71, Frimpong na Van Persie.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Sunderland ilikubali kipigo cha nyumbani cha 1-0 kutoka kwa Newcastle United, bao pekee la Ryan Taylor dakika ya 62.
Aston Villa iliikung’uta 3-1 Blackburn, mabao yake yakitiwa kimiani na Agbonlahor dakika ya 12, Heskey dakika ya 25 na Bent dakika ya 67, wakati bao la kufutia machozi la wapinzani wao lilitiwa kimiani na Pedersen dakika ya 52.
Everton ilifungwa nyumbani na 1-0 QPR, bao pekee la Tommy Smith dakika ya 31, wakati Swansea ililazimishwa sare ya bila kufungana na Wigan- na wakati tunakwenda mitamboni, mechi kati ya Chelsea na West Brom ilikuwa inaendelea.
Ligi hiyo inatarajiwa leo kwa mchezo mmoja kati ya Bolton na Man City kuanzia saa 12:00 jioni, wakati kesho mabingwa watetezi, Man Utd watamenyana na Tottenham kuanzia saa 4:00 usiku.



Comments