SIMBA YASHINDA, YANGA YAPAKATWA JESHINI

SIMBA imeanza vema Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuifunga JKT Oljoro mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha. Shukrani kwao kiungo Patrick Mutesa Mafisango raia wa Rwanda na mshambuliaji wa Kiganda, Emanuel Okwi wafungaji wa mabao hayo.
Hata hivyo, katika mchezo huo Simba ilipata pigo baada ya mshambuliaji wake Mzambia Felix Sunzu kupewa kadi nyekundu. Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, mabingwa watetezi Yanga walichapwa 1-0 na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro- bao pekee la mkwaju wa penalti la Kessy Mapande.
Toto African ya Mwanza inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake tatu na mabao matatu, ikifuatiwa na Simba, yenye pointi tatu na mabao mawili na Azam ya tatu kwa pointi zake tatu na bao moja, sawa na JKT ya nne. Juzi Coastal Union ya Tanga ilitoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar, sawa na Kagera Sugar na Ruvu Shooting, wakati Polisi Dodoma na African Lyon hazikufungana.
Mechi za leo zimekamilisha idadi ya mechi za ufunguzi za ligi hiyo- iliyotanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii, ambao Simba iliifunga Yanga 2-0, mabao ya Haruna Moshi na Sunzu.

Comments