SIMBA YANG'ARA, YANGA YANG'ANG'ANIWA MORO

Taita wa Yanga na Jaffar Gonga wa Moro United
SIMBA jana iliendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1- 0 dhidi ya Coastal Union katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.  Wakati mambo yakiwa shwari kwa Simba, kwa mtani wake Yanga, hali bado mbaya, baada ya jana kubanwa ‘mbavu’ na Moro United kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Moro United katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.  Katika mechi ya Mkwakwani, bao la Simba lilipatikana katika dakika ya 24 lililofungwa na Patrick Mafisango aliyefunga kwa shuti kali ambalo liligonga mwamba kabla ya kujaa wavuni.
Katika mechi hiyo, Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo kabla ya Coastal haijaonesha ‘uhai’ katika dakika za mwishoni mwa mchezo, lakini haikuambulia kitu licha ya washambuliaji wake kukosa nafasi kadhaa za kufunga kutokana na umaliziaji mbovu.
Katika mechi ya Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Yanga ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 68 lililofungwa na Haruna Niyonzima kwa kichwa baada ya kuunganisha vema krosi ya Godfrey Bony.
Dakika ya 87 Moro United ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Jarome Lambele aliyefunga bao hilo kwa shuti kali baada ya kuunganisha pasi ya Bakari Mpakala.
Lambele aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Benedict Ngassa. Mbali na kutoka sare, Yanga pia ilipomteza mchezaji wake Juma Seif ‘Kijiko’ aliyetolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu na mwamuzi Ibrahim Kidiwa baada ya kuunawa mpira katika eneo la hatari, awali Kijiko alikuwa na kadi ya njano.
Hiyo ni mechi ya pili kwa Yanga ambapo mechi ya kwanza ilifungwa bao 1-0 na JKT Ruvu.
Naye Mwandishi Wetu John Mhala anaripoti kuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
Arusha, timu ngeni kwenye ligi, JKT Oljoro ilipata ushindi wake wa kwanza baada ya kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0.
Bao la Oljoro lilifungwa na Rashid Roshua kwa kichwa baada ya uzembe wa beki ya Mtibwa Sugar kushindwa kuuondoa mpira kwenye eneo la hatari.
Naye Mwandishi Wetu Grace Chilongola anaripoti kutoka Mwanza kuwa Toto African imeendelea kushinda mechi zake baada ya jana kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Mfungaji wa Toto alikuwa Emmanule Swita aliyefunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 63 baada ya Paul Ngalema wa Ruvu kumwangusha Mwita Kenoronge katika eneo la hatari katika mechi hiyo Shaaban Suza wa Ruvu alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Chika Chuku wa Toto.
Kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera Sugar ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Villa Squard na kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Polisi ya huko imetoka sare ya mabao 2-2 na JKT Ruvu.



Comments