SIMBA, YANGA HAPATOSHI KESHO


NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho zitakabiliwa na patashika nzito, wakati watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba SC na Yanga watakapomenyana katika mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii, kuashiria kufunguliwa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Kwa mwaka huu pekee, huo utakuwa mchezo wa tatu kuwakutanisha watani hao wa jadi, kila timu ikiwa imeshinda mechi moja na kutoka sare mara moja pia, katika mechi tatu za mashindano tofauti.
Mapema Januari 12, mwaka huu katika fainali ya Kombe la Mapinduzi, Simba iliifunga Yanga mabao 2-0, wafungaji Mussa Mgosi dakika ya 33 na Shijja Mkinna dakika ya 71, wakati katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu msimu uliopita Machi 5, mwaka huu timu hizo zilitoka sare ya 1-1, Yanga wakitangulia kufunga dakika ya 59 kwa penalti ya Stefano Mwasyika baada ya Juma Nyosso kumkwatua Davies Mwape.
Hata hivyo, Mussa Mgosi aliyehamia DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), msimu huu, aliisawazishia Simba dakika ya 73, ingawa bao hilo lilizua utata kutokana na refa Orden Mbaga kwanza kwa kulikataa, kabla ya kulikubali baada ya kujadiliana na msaidizi wake namba moja.
Julai 10, mwaka huu tena katika fainali ya Kombe la Kagame, bao pekee la Mghana Kenneth Asamoah katika dakika ya 118, liiipa Yanga ushindi wa 1-0 kwenye uwanja wa Taifa.
Wakati huu leo ukiwa ni mchezo wa nne mwaka huu timu hizo kukutana, lakini pia unakuwa mchezo wa tano kwa timu kumenyana usiku na mara ya kwanza kukutana muda huo katika ardhi ya Bara.
Mechi zote nne za awali kuikutanihsa miamba hiyo usiku zilichezwa visiwani Zanzibar, kwenye Uwanja wa Amaan. Mechi ya kwanza kabisa ilikuwa ni Januari mwaka 1975 kwenye fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame na mabao ya Gibson Sembuli (marehemu) na Sunday Manara wakimtungua Athumani Mambosasa (marehemu) yaliipa Yanga ushindi wa 2-0.
Timu hizo zilikutana tena usiku Januari 1992 katika fainali ya michuano hiyo hiyo na dakika 120 ziliisha zikiwa zimefunga 1-1, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti na Simba ikashinda 5-4.
Mwaka huo huo, timu hizo zilikutana visiwani humo tena katika Ligi ya Muungano Oktoba 27 na bao pekee la Damian Mrisho Kimti liliwapa Wekundu wa Msimbazi ushindi wa 1-0. Mara ya mwisho watani hao wa jadi kukutana usiku ilikuwa ni Januari 12, mwaka huu katika fainali ya Kombe la Mapinduzi na mabao ya Mussa Hassan Mgosi dakika ya 33 na Shijja Mkinna dakika ya 71, yaliipa Simba ushindi wa 2-0.
Kocha Sam Timbe raia wa Uganda, leo atakuwa anaiongoza Yanga kwa mara ya tatu kucheza na watani wake hao wa jadi, akiwa na rekodi ya sare moja katika Ligi Kuu na kushinda mechi moja fainali ya Kagame.
Kwa Moses Basena raia wa Uganda pia, huu utakuwa mchezo wa pili kwake kukutana na Yanga tangu ajiunge na Simba, akiwa ana kumbukumbu ya kuchapwa bao 1-0 kwenye fainali ya Kombe la Kagame.

SIMBA SC:
Baada ya fainali ya Kombe la Kagame Julai 12, mwaka huu Simba walipata mapumziko ya wiki moja kabla ya kukutana tena wakianza na mazoezi ya ufukweni na gym mjini Dar es Salaam, kasha kwenda Zanzibar na wiki iliyopita walihamia Arusha ambako walicheza mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Victors ya Uganda waliyofungwa 1-0 na AFC Leopard ya Kenya waliyotoka nayo sare ya bila kufungana.
Simba ilirejea Dar es Salaam Jumapili na kuweka kambi katika hoteli ya Spice, Mtaa wa Lumumba, eneo la Mnazi Mmoja ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sigara, Chang’ombe.
Safu ya ushambuliaji ya Simba imeboreshwa kwa usajili wa washambuliaji wawili wapya, Mzambia Felix Sunzu na Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, ingawa imempoteza kinara wake wa mabao wa muda mrefu, Mussa Hassan Mgosi aliyehamia DC Motema Pembe ya DRC. Lakini leo, Sunzu atacheza na Haruna Moshi ‘Boban’ katika safu hiyo.
Mganda Emmanuel Okwi ambaye hakucheza Kombe la Kagame kutokana na kuwa Sweden kwenye majaribio, amerejea na leo anatarajiwa kuwamo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba akicheza sambamba na Sunzu na Boban.
Patrick Mutesa Mafisango anatarajiwa kuongoza safu ya kiungo pembeni yake akisaidiwa na Salum Machaku kulia na kushoto Okwi, wakati safu ya ulinzi ya Simba inatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa- Victor Costa Nampoka ‘Nyumba’ atasimama na Juma Said Nyosso wakati kiungo wa ulinzi atakuwa Jerry Santo.
Katika benchi la wachezaji wa akiba, watakuwapo Ally Mustafa ‘Barthez’, Salum Kanoni, Juma Jabu, Obadia Mungusa, Amri Kiemba, Shijja Mkinna, Uhuru Suleiman, Gervais Kago, Shomary Kapombe na Ulimboka Mwakingwe kama hali itaendelea vizuri, wakati Kelvin Yondan safari hii hata jezi hajapewa.

YANGA SC:
Baada ya kutwaa Kombe la Kagame, wachezaji wake walipewa mapumziko ya wiki moja kabla ya kukutana na kujifua kwa siku kadhaa, kasha kwenda Sudan kucheza mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya wenyeji wao, El Hilal wanaonolewa na kocha wao wa zamani, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’.
Katika mechi hizo zote, Yanga ilifungwa mabao 3-1 kila mechi na kurejea Dar es Salaam kujipanga upya wakiendelea na mazoezi kwenye Uwanja wao wa Kaunda, Jangwani walipoweka kambi kwenye hosteli yao iliyokarabatiwa na milionea Yussuf Manji.
Katika mazoezi yake, kocha Timbe amekuwa akiwazuia mashabiki kuingia kutazama akihofia mbinu zake kuibwa na mara nyingi amekuwa akiwapa mazoezi wachezaji wake wakati wa asubuhi tu.
Kipa namba moja wa Yaw Berko leo hatakuwapo kabisa kutokana na kuwa majeruhi na kwa mara ya kwanza Shaaban Hassan Kado atadaka kwenye mechi ya watani wa jadi, kulia akilindwa na Nsajigwa Shadrack, kushoto Oscar Joshua katikati Chacha Charles Marwa ‘CCM’ na Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’.
Kiungo wa ulinzi ataanza Juma Seif ‘Kijiko’ wakati kiungo mchezeshaji ataanza Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ kulia akisaidiwa na Godfrey Taita na kushoto Kiiza Hamisi wakati safu ya ushambuliaji itaundwa na Jerry John Tegete na Kenneth Asamoah Boateng.
Katika benchi watakuwapo Said Mohamed, Freddy Mbuna, Abuu Ubwa, Zubery Ubwa, Rashid Gumbo, Nurdin Bakari, Pius Kisambale, Shamte Ally, Idrisa Rashid na Julius Mrope.
Kwa kawaida, mechi za Ngao, baada ya dakika 90 kama timu zitakuwa hazijafungana, sheria ya mikwaju ya penalti hufuatia moja kwa moja na mwaka jana pia ilikuwa hivyo, lakini safari hii TFF wamesema itakuwa dakika 120. Je, mambo yatakuwaje leo? Tusubiri tuone.



Comments