NGORONGRO YAALIKWA COSAFA

TIMU ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) imealikwa kushiriki michuano ya umri huo ya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwaka Afrika (Cosafa) itakayofanyika kuanzia Desemba 1 jijini Gaborone, Botswana.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura ilieleza kuwa michuano hiyo itamalizika Desemba 10 mwaka huu.
“Wachezaji wanaotakiwa kushiriki michuano hiyo ni wale waliozaliwa baada ya Januari 1, 1992. “Timu zinatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kufikia Agosti 17 mwaka huu na ratiba itapangwa Agosti 24 mwaka huu,” alisema Wambura.
Mwezi uliopita timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ nayo ilishiriki michuano ya Cosafa iliyofanyika Harare, Zimbabwe na kushika nafasi ya tatu.
Twiga Stars ilikuwa ikishiriki michuano hiyo ikiwa timu mwalikwa, ambapo timu nane zilishiriki wakiwemo wenyeji Zimbabwe.
Nyingine zilikuwa ni Lesotho, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji na Malawi.

Comments