NASRI ATUA MAN CITY

ILE ngoma ya ‘nataka sitaki’ iliyokuwa inachezwa na Arsene Wenger, hatimaye imefikia ukingoni na kukubali kumuuza mchezaji wake tegemeo Samir Nasri kwa Manchester City. Jana jioni, Wenger aliamua kuafikiana na matakwa ya Manchester City, ambayo imemnunua mchezaji huyo kwa kiasi cha pauni milioni 24 (Sh bilioni 64).
Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa, mwenye miaka 24, jana usiku alitarajiwa kwenda katika Jiji la Manchester kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya yake na hatakuwemo katika kikosi kitakachoivaa Udinese.
Arsenal, kudhihirisha imekubaliana na hilo, jana ilitoa taarifa rasmi ikisema imekubaliana na Samir Nasri na kwa sasa anaruhusiwa kwenda Manchester City.
“Arsenal imekubaliana na Samir Nasri na kwa sasa anaweza kwenda Manchester City na kiungo huyo hatakuwemo katika kikosi kitakachoivaa Udinese na kwa sasa anakwenda kupimwa afya yake.
“Kila kitu kitakamilika iwapo Nasri atafuzu vipimo na kama akifuzu baada ya hapo mambo yote yatamalizika,” ilisema sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.
Nasri jana asubuhi alifanya mazoezi ya pamoja na Arsenal na hivyo kuanza kutia shaka kama kweli nia yake ya kujiunga na Manchester City itatimia.
Wenger alikiri kuuzwa kwa Nasri na kusema kwa sasa kila kitu kinakwenda kukamilika na hawezi kuzuia jambo hilo kutendeka.

Comments