MISS PHOTOGENIC KUPATIKANA KESHO ARUSHA

MASHINDANO ya kumsaka mrembo bora katika picha (Vodacom Miss Photogenic) yatafanyika kesho kwenye Corridor Spring Hotel mkoani Arusha, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim “Uncle” Lundenga amesema.

Lundenga amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha warembo wote 30 walipo katika ziara ya mbuga za wanyama mkoani rusha na Manyara na mshindi atafuzu moja kwa moja hatua ya nusu fainali ambayo ujumuisha warembo 15.
Alisema kuwa kinyang’anyiro hicho ni kigumu zaidi na tayari majaji wanakazi kubwa ili kuweza kumpata mrembo bora wa katika muonekano wa picha.
“Ni mashindano magumu ambayo yameshirikisha warembo wote 30, hauwezi kutabiri, tunaamini majaji watafanya kazi ipasavyo ili kumpata mshindi wa kweli,” alisema Lundenga.
Tayari mwakilishi kutoka kanda ya Temeke, Mwajabu Juma amefuzu nafasi hiyo ya 15 bora baada ya kutwaa taji la mrembo bora katika maonyesho ya mavazi “Miss Top Model” lililofanyika siku ya pili mara baada ya kuingia kambini.
Mbali ya mashindano hayo, warembo hao pia watashindana katika taji la vipaji, Mrembo bora wa michezo na mrembo mchangamfu, mwenye ushirikiano na nidahmu bora (Miss Personality). Warembo hao wote watafuzu hatua ya 15 bora siku ya shindano hapo Septemba 10 kwenye ukumbi wa Mlimani City.
Wakati huo huo; Lundenga amesema kuwa ziara yao ya mikoani imelenga kudadi utalii wa ndani na kuwahamasisha Watanzania kuwa na tabia ya kutembelea vivutio vya utalii nchini.
Mbali ya lengo hilo, ziara hiyo pia imelenga kuwapa ufahamu warembo kuhusiana na mila mbali mbali za makabila tofauti ya hapa nchini.
Alisema kuwa hatua waliyofikia, imewapa faraja kubwa na warembo wamejionea vitu mbali mbali na kuamini watakuwa mabalozi wazuri mara baada ya mashindano yao na hata katika mashindano ya Dunia.
“Kwa mara ya kwanza warembo wameona jinsi Simba akifukuza na kula mnyama mwenzake, vitu hivyo walikuwa wanaona kwenye televisheni tu, wamejifunza mambo mengi,” alisema.

Comments