KIIZA AWALIZA YANGA


UONGOZI wa klabu ya Yanga jijini Dar es Salaam umesema umesikitishwa na kitendo alichokifanya nyota wake wa kimataifa kutoka nchini Uganda, Hamis Kiiza kuondoka nchini bila ya kutoa taarifa kwa kiongozi yeyote.

Ofisa habari wa timu hiyo, Luis Sendeu alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa uongozi huo umesikitishwa na kitendo hicho na upo kwenye tafakari na utatoa taarifa hatua utakazozichukua kuhusiana na kitendo hicho.
"Kwa kweli tumesikitishwa na kitendo hicho alichokifanya Kiiza kuondoka bila ya kuaga mtu yeyote, tulipata taarifa akiwa ameshafika uwanja wa ndege Mwl. Julius Nyerere tayari kuanza safari ya kurejea nchini kwao Uganda," alisema Sendeu.Alisema uongozi kwa sasa utakutana ili kuweza kutafakari na baadaye kutoa uamuzi mgumu kuhusiana na suala hili na kuwa fundisho kwa wengine.
"Tumepata taarifa kuwa amefika Uganda, lakini hajawasiliana na kiongozi yeyote kusema sababu zilizomfanya aondoke bila kuaga mtu yeyote yule, huku akitambua yeye ni mwajiriwa wa Yanga," aliongeza.
Hata hivyo; alisema Chama cha soka nchini Uganda kiliitumia Yanga barua pepe (E-mail) kwa ajili ya kumtaka Kiiza kujiunga na timu ya Taifa ya Vijana U-23, kwenda kushiriki Michezo ya Afrika 'All Afrika Games' itakayofanyika Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3 hadi 18 mwaka huu.
"Tunajaribu kufanya naye mawasiliano ili kujua kilichomkuta mpaka kuamua kuondoka bila kuaga, lakini hatujafanikiwa, hatuwezi tukamchukulia hatua za kinidhamu mpaka pale pande zote zitakapokutana na kujua kilichomsibu," alisisitiza.
Aidha alisema wanahisi mchezaji huyo alipata taarifa za kushtua kutoka kwenye familia yake kutokana na kuuguliwa na mchumba wake pamoja na mjomba."Labda amepata taarifa mbaya zilizomfanya kuchanganyikiwa na kuondoka bila ya kujitambua," alihisi.Wakati kuondoka kwa nyota huyo kukibaki kuwa ndoto, kuna tetesi kuwa mchezaji huyo alikuwa hajakamilishiwa fedha zake zote za usajili kuichezea klabu hiyo msimu huu.
Sendeu alikiri kuwa ni kweli mchezaji huyo amejiunga kuichezea Yanga kwa mkataba wa miaka miwili, lakini hajamaliziwa fedha zake zote isipokuwa makubaliano yao ni kulipana kwa kila mwaka.Katika hatua nyingine kocha mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe ameshindwa kufanya mazoezi na timu hiyo kutokana na hali yake kiafya kuwa sio nzuri.
"Kocha leo (jana) ameshindwa kufanya mazoezi na timu kutokana na kujihisi vibaya kiafya na msaidizi wake Fred Minziro ndiye alichukua jukumu hilo kwa leo (jana) kusimamia programu ya mazoezi," alisema.
Hata hivyo mshambuliaji Davies Mwape aliyekuwa majeruhi wa nyama za paja amejiunga na wenzake jana na kuanza mazoezi ya kujiandaa na pambano la Ngao ya Hisani dhidi ya watani wao Simba Agosti 17, lakini Nurdin Bakari bado ameshindwa kujiunga na wenzake.



Comments