KIIZA AREJEA, YANGA SASA KAMILI


KIUNGO wa Yanga, Hamis Kiiza aliyekuwa ametimkia kwao Uganda bila kuutaarifu uongozi amerejea Dar es Salaam.  Ofisa Habari wa Yanga, Luios Sendeu alisema kuwa Kiiza aliwasili jana alasiri na moja kwa moja kupelekwa kambini waliko wachezaji wenzake kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Simba wa Ngao ya Jamii kesho.  “Kiiza tayari amewasili, hayo mambo mengine kwa sasa tuyaache kwanza, akili zetu zipo katika mchezo na Simba,” alisema Sendeu.
Alitoa kauli hiyo kutokana na swali aliloulizwa na gazeti hili kuhusiana na hatua ambazo itamchukulia Kiiza kwa kuondoka bila ruhusa.
Mshambuliaji huyo mpya wa Yanga maarufu kama ‘Diego’, aliondoka kwenda kwao Uganda mara baada ya Yanga kuwasili Dar es Salaam ikitokea Khartoum, Sudan, ambako ilienda kujipima nguvu na Al Hillal.
Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa mshambuliaji huyo kuzua kizaazaa katika klabu hiyo, mara ya kwanza ilikuwa wakati aliposhindwa kuripoti kambini kuanza mazoezi ya pamoja ya kujiandaa na msimu wa wa ligi na kuwasili Dar es Salaam siku chache kabla timu haijaenda Sudan.



Comments