GUNNERS KAZINI ULAYA USIKU HUU


THE GUNNERS, wanajikuta kwenye mtihani mwingine baada ya ule wa kwanza kwenye ligi kuu ya England dhidi ya Newcastle United . Safari hii bunduki zinaelekezwa kwa klabu ya Calcio Udinese kwenye mchezo wa kufuzu kuingia hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa . Arsenal wanaingia kwenye mchezo huu huku wakijua kuwa wakiteleza kidogo watawanyima mashabiki wao raha ya kushuhudia timu yao ikipambana na timu bora barani Ulaya lakini pia watajinyima mapato muhimu yatokanayo na kushiriki ligi ya mabingwa . Bado hali ya kambi ya Arsenal kuelekea kwenye mchezo muhimu kama huu si shwari kutokana na kuondoka kwa Cesc Fabregas japo baadhi ya mashabiki wanaona kuwa bora ameondoka na wamebaki kwa amani kwani hisia za Fabregas kutojitolea kwa asilimia 100% akiwa Arsenal zilikuwa zinaonekana.
Arsene Wenger ana kazi kubwa ya kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake na kuwapa ujasiri wa kupambana na Udinese .
Ni vyema wachezaji wa Arsenal wakatambua kuwa wanao uwezo wa kupata mafanikio makubwa ila wanalazimika kuwa na ujasiri wa kupambana kiume na kuacha kucheza soka la kitoto ambalo limewafelisha mara kadhaa nyuma.
Kuelekea mchezo dhidi ya Udinese, Arsene Wenger anataraji kupanga kikosi ambacho si tofauti na kilichocheza dhidi ya Newcastle , ila badiliko kubwa litakuwa kumkosa nahodha mpya Robin Van Persie ambaye amefungiwa michezo miwili baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Barcelona msimu uliopita .
Hii inamaanisha kuwa Arsenal wataanza na Theo Walcott kwenye nafasi ya Van Persie akisaidiana na Gervinho .
Kwenye upande wa ulinzi Arsenal wataendelea kuwatumia Bacary Sagna , Kieran Gibbs , Thomas Vermalaen na Laureant Koscielny ambao wameonyesha uhai mkubwa uliokosekana kwa muda mrefu kwenye ‘back-four’ ya Arsenal.
Thomas Vermalaen alikuwa mtulivu sana kwenye mechi dhidi ya Newcastle akimuongoza mwenzie Koscielny kwa umakini mkubwa jambo ambalo liliwapa wakati mgumu washambuliaji wa Newcastle kina Shola Ameobi.
Changamoto kubwa kwa watu hawa ni ukweli kuwa Shola Ameobi ni mnyama tofauti na Antonio Di Natale anayeongoza mashambulizi ya Udinese .
Kwenye safu ya viungo tatizo la Nasri na Fabregas linaweza kuwa gumu kulipatia ufumbuzi kwa mzee Wenger, na hii inatokana na kukosekana kwawachezaji wengine wengine muhimu kama Jack Wilshere na Abou Diaby wote wakisumbuliwa na majeraha mbalimbali waliyopata wakati wa mechi za ‘pre-season’ .
Hali hii itamlazimu Wenger kuendelea kuwatumia viungo Alex Song au Emmanuel Frimpong kwenye nafasi ya kiungo wa kukaba na Aron Ramsay kama kiungo mbunifu atakayeendesha safu nzima ya mbele kwa timu yake akisaidiwa na Tomas Rosicky iwapo atapasi vipimo vya ‘fitness’ baada ya kutonesha jeraha la ‘groin’ siku ya jumamosi.
Ni muhimu kwa Arsene Wenger kuendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1na kumpa uhuru wa kutengeneza nafsi kiungo Aron Ramsay japo hakucheza vizuri sana siku ya jumamosi na kama itabidi basi Wenger hana budi kumpa nafasi Mmorocco Marouanne Chamakh kwenye safu ya usahmbuliaji .
Kwa upande wa Udinese kuna tatizo kama la Arsenal nalo ni kuondoka kwa wachezaji kadhaa tegemeo , muhimu zaidi Alexis Sanchez aliyesajiliwa na Barcelona na Cristian Zaporta ambaye ameenda Villareal.
Wachezaji hawa wameacha pengo ambalo halitakuwa rahisi kuziba sana kwa Sanchez.
Mashambulizi ya Udinese yataongozwa na Antonio Di Natale ambaye ndiye nahodha na mchezaji muhimu aliyebakia baada ya kuondoka kwa Alexis Sanchez .
Pamoja na kumpoteza winga huyu toka Chile bado Udinese kama timu wanabaki kuwa kikosi chenye uwezo mkubwa wa kuidhuru Arsenal .
Di Natale alikuwa mfungaji bora wa Serie A kwenye msimu uliopita na ni mshambuliaji mwenye sifa zote za ukamilifu kama mshambuliaji na atawapa wakati mgumu mabeki wa Arsenal .
Udinese wanashambulia sana kwa kutumia ‘wings’ na wanatumia mfumo wa 3-4-3 huku mabeki wa pembeni kama beki toka Chile Mauricio Isla na mwenzie Pablo Armero toka Colombia wakipanda kusaidia mashambulizi kwa kasi kubwa .
Udinese pia wana kipa mwenye uwezo mkubwa sana ambaye mara nyingi husahaulika miongoni mwa makipa wa Serie A Samir Handanovic mtu ambaye aliwahi kuhusishwa na kusajiliwa Arsenal siku za nyuma .
Handanovic anasaidiwa na beki makini wa kati Mehdi Benatia na kwenye kiungo cha kati yuko Mghana Kwadwo Asamoah , mwafrika ambaye anapenda sana mapmbano ya kutumia nguvu kwenye eneo la katikati ya kiwanja.
Na mwisho wa siku itakuwa ni vita ya mbinu baina ya Professa Arsene Wenger na mwenzie Francesco Guidoline ambao wataviongoza vikosi vyao kwenye mchezo wa leo japo Arsenal watamkosa kocha wao ambaye anatumikia kifungo baada ya kumtolea maneno machafu mwamuzi Massimo Bussaca .
Ni mchezo wa dakika 180 muhimu kwa Arsenal ambao unaweza kutengeneza au kuharibu kabisa msimu wao kwa kuwa wataucheza wakiwa na presha ya kufuzu kucheza ligi ya mabingwa kuliko Udinese ambao kwenye mchezo huu wanaingia kama ‘Underdogs’.

Vikosi vinaweza kuwa hivi
ARSENAL
Szczesny, Sagna, Koscielny, Vermaelen, Gibbs, Rosicky, Song, Ramsey, Gervinho, Walcott na Arshavin
UDINESE
Handanovic, Domizzi, Larangeira, Benatia, Isla, Pinzi, Asamoah, Doubai, Armero, Di Natale na Barreto

Comments