GURUMO KURUDI JUKWAANI IDD MOSI


Baada ya kutoonekana jukwaani kwa muda mrefu kutokana na kuugua, mwanamuziki nguli hapa nchini Muhidin Gurumo anatarajia ataonekana  tena kwenye jukwaa la Msondo Ngoma siku ya Iddi Mosi wakati bendi hiyo itakapotumbuiza kwenye bonanza maalum la Konyagi litakayofanyika kwenye viwanja vya TCC Club, Chang’ombe.
Bonanza hilo litatumiwa na bendi hiyo vile vile kusheherekea ushindi wa tuzo ya bendi bora ya muziki wa rumba Afrika Mashariki na Kati,iliyoipata baada ya kuzibwaga bendi zingine zikiwemo zile zinazoongozwa na wanamuziki magwiji kutokaCongo kama vilE JB Mpiana na Werason Ngiama Makandi, kwenye tuzo zilizofanyika Nairobi , Kenyahivi karibuni.
Kwa kipindi cha takribani miezi sita wapenzi wa bendi hiyo wamekosa sauti ya mwanamuziki huyo kutokana na kuugua.
“Tunaomba wapenzi wetu wajitokeze kwa wingi kwani tumewaandalia vitu vizuri siku ya Iddi Mosi,” alisema kiongozi wa bendi hiyo, Saidi Mabera.
Bonanza hilo ambalo litafanyika kuanzia saa nane mchana, limeandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts chini ya udhamini wa Konyagi.
Mratibu wa bonanza hilo , Joseph Kapinga, amesema kuwa Msondo Ngoma pia italitumia onyesho hilo kupromoti albamu yao mpya ijulikanayo kama Huna Shukrani.
Nyimbo zilizo katika albamu hiyo ni Huna Shukraniuliotungwa na Saidi Mabera, Cheo ni Dhamana(Eddo Sanga),  Kiapo (Hussein Jumbe), Mama Kosi(Joseph Maina), Machimbo (DJ Papa Upanga) na Haki Yangu Iko Wapi  (H. Huvuruge).
Pia wapenzi wao  wataburudika na nyimbo zao za zamani kana Kilio Cha Mtu Mzima, Kaza Moyo, Piga Ua Talaka Utatoa na nyinginezo. Pia Zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washabiki na Konyagi.


Comments