FERGIE AMSHITUA WENGER, AFANYA USAJILI WA NGUVU

KIPIGO cha mabao 8-2 ilichotoa kikosi cha Manchester United iliyo chini ya Alex Ferguson, kimemshitua Arsene Wenger na jana amekamilisha taratibu za kutwaa wachezaji wawili waje kuimarisha ukuta wa Arsenal. Wenger mpaka tunakwenda mitamboni alikuwa katika hatua za mwisho za kumnasa beki wa kati wa kimataifa wa Ujerumani, Per Mertesacker na alikuwa tayari kutoa kiasi cha pauni milioni 8 ili kumtwaa.
Wakati akifanya jitihada za mwisho za kuwania kabla dirisha la usajili halijafungwa, huku mchezaji huyo akiwasili London kwa vipimo vya afya, tayari Wenger amemtwaa beki wa kushoto wa Brazil, Andre dos Santos kwa pauni milioni 6.2.
Dos Santos alitua ghafla jana jijini hapa, ambapo alipelekwa moja kwa moja kwenda kufanyiwa vipimo vya afya na alifnikiwa kufuzu na kusainishwa mkataba wa miaka minne wa kuichezea timu hiyo.
Dirisha la usajili ambalo limebakiza saa chache kabla ya kufungwa, linaonekana kumtesa Wenger, kwani alitua Chelsea na kuwaambia anawapa pauni milioni 8 ili wamuachie Florent Malouda.
Sio tu Malouda, bali anamtaka pia na beki mwingine wa timu hiyo Alex, huku akitaka kuimarisha kiungo kwa kuhakikisha anakuwepo Yossi Benayoun.
Chelsea imewaambia Arsenal, kama wanamtaka Alex wanapaswa kulipa pauni milioni 10, ambazo Wenger amekataa na kudai anaweza kuuzwa chini ya kiwango hicho.
Naye Mertesacker ambaye anaichezea Werder Bremen, alikuwa London jana mchana na alikuwa katika hatua za mwisho za kusajiliwa na timu hiyo kabla ya dirisha la usajili kufungwa leo usiku.

Comments