CHELSEA YASHINDA, DROGBA AUMIZWA

MABAO ya dakika za jioni jana yaliipa Chelsea ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Norwich, waliokuwa wakicheza 10, kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Timu hiyo inayofundishwa na Andre Villas-Boas, ilikuwa hatarini kulazimishwa sare na Norwich, iliyopanda Ligi Kuu msimu huu wakati Grant Holt alipowaadhibu kwa makosa ya kipa wa Blues, Hilario na kulipa bao la Chelsea lililofungwa na Jose Bosingwa.
Chelsea ilipata pigo baada ya mshambuliaji wake Didier Drogba kuumia ‘vibaya’ mapema tu na kutoka nje baada ya kugongana na kipa wa Norwich, John Ruddy.
Lakini Lampard aliihakikishia Chelsea ushindi kwa mara ya pili, katika mechi tatu za ligi chini ya kocha Villas-Boas, alipofumua shuti kali zikiwa zimebaki dakika nane, kabla ya Juan Mata kufunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na Blues akitokea Valencia dakika ya mwisho kabisa.
Chelsea ilipata bao la kwanza dakika ya sita, mfungaji akiwa beki wa kulia wa Kireno, Bosingwa ambalo lilikuwa bao lake la kwanza tangu Novemba mwaka 2008, akifumua shuti kali la mbali.
Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 63, wakati Holt aliposawazisha akitumia vema uzembe wa kipa Mreno, Hilario, aliyekuwa amemshikia nafasi ya majeruhi Petr Cech jana— ambaye alitoka bila mahesabu langoni na kupishana na krosi ya Wes Hoolahan, Holt kutumbukiza mpira nyavuni langoni kukiwa hakuna mtu.
Bao hili lilifuatiwa na pigo lingine kwa Chelsea, wakati Drogba alipoumia baada ya kugongana na Ruddy, hivyo mchezo kusimamishwa kwa dakika saba wakati nyota huyo wa Ivory Coast akitibiwa.
Hata hivyo, Lampard alifunga bao la pili kwa penalti, baada ya Ruddy kutolewa kwa kadi nyekundu kutokana na kumuangusha Ramires na winga wa Hispania, Mata.
Katika mchezo mwingine jana, Blackburn ilipoteza penalti mbili kisha wakaizawadia penalti Everton iliyoshinda 1-0, kwenye Uwanja wa Ewood Park.
Rovers walipata nafasi ya kuongoza mechi hiyo mapema kipindi cha pili, wakati Tim Howard alipookoa mkwaju wa penalti wa Junior Hoilett, baada ya Mauro Formica kumchezea rafu Ross Barkley.
Formica alikosa penalti aliyoitafuta mwenyewe— akipiga shuti kwenye mwamba, baada ya kufanyiwa faulo na Phil Jagielka katika dakika ya mwisho.
Everton waliwaadhibu wapinzani wao hao kwa makosa yao hayo, wakati kiungo wa Hispania, Mikel Arteta, alipowafungia wenyeji bao dakika ya 90 kwa penalti ya utata waliyozawadiwa na Lee Mason, baada ya Chris Samba kumchezea rafu Marouane Fellaini.
Swansea ililazimishwa sare ya bila kufungana nyumbani kwa mara ya pili mfululizo na Sunderland kwenye Uwanja wa Liberty.
Wigan iliendeleza rekodi yake ya kutofungwa kutokana ushindi wa 2-0 uliotokana na mshambuliaji wa Argentina, Franco Di Santo dhidi ya QPR.
Wolves nayo iliendeleza ubishi wa kufungwa baada ya timu hiyo ya Mick McCarthy kutoka sare ya bila kufungana na Aston Villa.
Wakati tunakwenda mitamboni, mechi kati ya Liverpool na Bolton ilikuwa inaendelea, wakati leo mabingwa watetezi, Manchester United wanamenyana na Arsenal na Manchester City watasafiri kuifuata Tottenham. Mechi nyingine leo ni kati ya Newcastle na Fulham na West Brom dhidi ya Stoke.

Comments