AZAM YALAMBWA CHAMAZI

IKIWATUMIA nyota wake wote; Kipre Herman Tchetche wa Ivory Coast, Nafiu Awudu na Yahya Wahab wa Ghana na Mrisho Ngassa, timu ya Azam FC imeshindwa kutamba mbele ya African Lyon, baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Dar es Salaam.
Azam kabla ya kuanza kwa ligi hiyo ilifanya ziara ya kimataifa nchini Uganda na Rwanda na kucheza mechi mbalimbali za kirafiki na timu kubwa za huko, ikiwa ni sehemu mojawapo ya maandalizi yao.
Katika mchezo wao wa kwanza Azam walifanikiwa kuifunga Moro United bao 1-0, ambapo African Lyon walilazimishwa sare ya bila kufungana na Polisi Dodoma. Katika mchezo huo wa jana timu hizo zilianza kwa kusomana huku zikishambuliana kwa zamu, dakika ya sita mshambuliaji wa Azam, John Bocco itabidi ajilaumu kwa kukosa bao la wazi baada ya kupiga shuti kali, lakini kipa wa Lyon, Noel Mulosi alipangua shuti hilo.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu zote kutoka suluhu, kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko kwa wachezaji wao, dakika ya 49 Bocco alikosa bao lingine la wazi baada ya kubaki yeye na kipa na kupiga shuti kali ambalo liligonga mwamba.
Mpira uliendelea huku kila timu ikijitahidi kutafuta bao, dakika ya 57 African Lyon walifanya shambulizi moja la nguvu, lakini mshambuliaji wake, Tino Augustino alipaisha mpira juu akiwa yeye na kipa.
Hata hivyo Azam jana walionekana kupooza sana tofauti na mashabiki walivyotarajia, dakika ya 86 African Lyon walipata bao kupitia kwa mshambuliaji wake Adam Kingwande, baada ya kupata mpira wa krosi iliyochongwa vizuri na Tino Augustino.
Bao hilo liliwaongezea kasi Lyon, ambao walianza kufanya mashambulizi ya nguvu kwenye lango la Azam, dakika ya 89 almanusra Lyon waongeze bao la pili kupitia kwa mshambuliaji wao, Tino lakini akiwa yeye na kipa alipaisha mpira juu. Katika mchezo huo, Azam FC ilipata pigo dakika ya 75, baada ya kiungo wake, Salum Abubakar kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Adam Kingwande. Hata hivyo, Azam itabidi wampongeze kipa wao Mserbia Obren Curkovic ambaye alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa mabao mengi ya wazi.



Comments