AZAM YAANZA VEMA CHAMAZI, TOTO YAFANYA KUFURU MWANZA


TIMU za soka za Azam FC na Toto African ya Mwanza  zimeanza vizuri, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambapo Azam wameifunga Moro United bao 1-0 na Toto wameimwagia mvua ya mabao 3-0, Villa Squad. Kwa upande wa Azam FC na Moro mchezo wao ulichezwa Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya Dar es Salaam. Mpira huo ulianza kwa timu zote mbili kushambuliana, dakika ya 12 mchezaji wa Azam Ramadhan Chombo 'Redondo' aliikosesha bao timu yake baada ya kupiga mpira wa adhabu ndogo ulioenda moja kwa moja wavuni, lakini kipa wa Moro akaudaka na kuutema kabla ya mabeki wake kuuokoa tena.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana dakika ya 27 Gaudence Mwaikimba wa Moro United alikosa bao la wazi, ni baada ya kupiga shuti kali lililogonga mwamba na mpira kurudi uwanjani, dakika ya 44 John Bocco wa Azam anaipatia timu yake bao la kwanza alilofunga kwa penalti baada ya mchezaji huyo kuangushwa eneo la hatari na beki wa Moro Tumba Swedi.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Azam walikuwa mbele bao 1-0.Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kufanya mabadiliko kwa wachezaji wake,Azam walianza kwa kasi ambapo dakika ya 52 Bocco anakosa bao la wazi baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Kipre Tchetche lakini anachelewa kuupata mpira huo na kipa wa Moro anauwahi.
Kwa upande wa Moro nao kosa kosa zinakuwa nyingi baada ya mshambuliaji wake aliyetokea benchi Jerome Lambele ambaye alichukua nafasi ya Sultan Kasikasi kushindwa kufunga bao akiwa yeye na kipa tu dakika ya 55, mpira ulimalizika kwa bao 1-0.
Mwandishi wetu, Christopher Gamaina anaripoti kutoka Mwanza kuwa, Toto African imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Villa Squad, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM, Kirumba.
Mabao ya Toto yalifungwa na Mohammed Hassan dakika ya 29 na Mnigeria Enyima Darington ambaye alifunga mawili dakika ya 56 na 75, katika mchezo huo mchezaji wa Villa Mohammed Said anazawadiwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Toto.
Kwa upande wa Tanga, timu ya Coastal Union na Mtibwa Sugar zimetoka sare ya bao 1-1, mchezo huo umechezwa Uwanja wa Mkwakwani, Coastal ndio walioanza kufunga bao dakika ya 13 kupitia kwa mchezaji wao Sabry Ally, kabla ya Mtibwa Sugar kusawazisha dakika ya 45 kupitia kwa Hussein Javu.
Kwa upande wa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba timu ya Kagera Sugar na Ruvu Shooting zimetoka sare ya bao 1-1, Ruvu ndio walioanza kupata bao dakika ya 10 kupitia kwa mshambuliaji wao Abdallah Juma, Kagera walisawazisha bao hilo dakika ya 45 kupitia kwa mshambuliaji wao David Charles, katika mchezo huo mchezaji wa Ruvu Hassan Salehe alizawadiwa kadi nyekundu dakika ya 46 baada ya kumchezea rafu Mau Bofu wa Kagera. Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma timu ya Polisi Dodoma na African Lyon zimetoka suluhu.

Comments