AFRICAN LYON KULIPA WACHEZAJI KWA MAKATO

Timu ya African Lyon imeomba kuwalipa kwa makato ya mlangoni wachezaji wake wawili wanaoidai; Godfrey Komba na Abdul Masenga ambao ilikatiza mikataba yao msimu uliopita. Awali Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliiagiza Lyon kuwalipa wachezaji hao kufikia Agosti 17 mwaka huu vinginevyo isingeruhusiwa kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom inayoanza leo (Agosti 20 mwaka huu).
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliitaka Lyon ithibitishe kwa maandishi kuwa itakatwa kwenye mapato yake ya mlangoni katika mechi hadi deni la wachezaji hao litakapomalizika. Lyon imetekeleza maagizo hayo, hivyo imeruhusiwa kucheza mechi yake ya leo (Agosti 20 mwaka huu) dhidi ya Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Hivyo Lyon itakatwa katika mechi yake ya leo ili kulipa deni hilo. Kama fedha ilizopata katika mgawo hazitatosha kulipa deni hilo itakatwa sehemu iliyobaki katika mechi inayofuata.
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji katika kikao chake cha Januari 7 mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa kiliiagiza Lyon iwalipe wachezaji hao baada ya kusitisha mikataba yao nje ya taratibu za kimikataba. Masenga na Komba kila mmoja anadai sh. milioni 4.3.
Wachezaji hao wataarifiwa juu ya utaratibu wa malipo yao ambapo TFF ndiyo itakayofanya makato kwa niaba yao.

FIFA YARUHUSU ITC YA KAGO ITOLEWE
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) limeruhusu Shirikisho la Mpira wa Miguu Jamhuri ya Afrika ya Kati kutoa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Gervais Anold Kago aliyejiunga na timu ya Simba kutoka Olympic Real de Bangui ya huko.
FIFA imeruhusu ITC itolewe baada ya kubaini kuwa Simba ilituma maombi ya kuomba hati hiyo ndani ya muda uliopangwa, lakini CAR ilishindwa kufanyia kazi. Hivyo kinachosubiriwa sasa ni CAR kutuma ITC hiyo.
Licha ya FIFA kuagiza hivyo, TFF imeitaka Simba kukata jina moja kati ya sita ya wachezaji wa kigeni ilionao katika orodha yake. Kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom inaruhusu timu kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi watano.
Wachezaji wa kigeni ambao Simba ina mikataba yao ni Derrick Walulya, Emmanuel Okwi, Felix Sunzu, Gervais Kago, Patrick Mafisango na Jerry Santo.
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji wakati ikipitia usajili iliagiza kuwa Walulya ambaye Simba ilisema imemuacha ni mchezaji wake kwa vile bado ina mkataba nayo. Hivyo inachotakiwa kufanya Simba ni kuvunja mkataba wa mchezaji mmoja ili kubaki na watano.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Comments