YANGA HUREEEEEEEEEEE

YANGA ya Dar es Salaam, jana ilikata tiketi ya kuingia Robo Fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Castle, kama vinara wa Kundi B, baada ya kuwalaza mabingwa wa Uganda, Bunamwaya mabao 3-2, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa mchezo huo alikuwa ni mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Davies Mobby Mwape, aliyeifungia Yanga bao la ushindi dakika ya pili ya muda wa nyongeza, baada ya kutimu kwa dakika 90 za kawaida za mchezo huo.
Yanga imeungana na El Merreikh ya Sudan kuingia Robo Fainali kutoka kundi hilo, lililokuwa gumu, ambayo imemaliza na pointi tano na kushika nafasi ya pili, wakati Bunamwaya waliomaliza na pointi nne wanashika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo na Elman ya Somalia imeondoka mikono mitupu, haina pointi wala bao hata moja, zaidi ya kubugizwa jumla ya mabao tisa katika mechi tatu.
Yanga sasa itashuka dimbani Julai 5 kumenyana na ama Simba au Zanzibar Ocean View, itategemea na matokeo ya mechi za leo za Kundi A.
Merreikh watamenyana na Ulinzi ya Kenya Julai 4 na Simba kama wataendelea kukaa kileleni mwa kundi hilo, basi watamenyana na APR ya Rwanda, katika Robo Fainali ambao wamepita kama washindi wa pili bora kutoka kundi B na C.
Vinara wa Kundi C, St George ya Ethiopia, watamenyana na mshindi wa pili wa Kundi A Julai 5, nafasi ambayo kabla ya mechi za leo, inashikiliwa na Zanzibar Ocean View.
Katika mchezo wa jana uliokuwa mkali na wa kusisimua, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 26, mfungaji akiwa ni mshambuliaji wake Mganda, Kizza Hamisi ‘Diego’, baada ya mabeki wa Bunamwaya, Kisaliita Ayubu na Seku Ronald kujichanganya.
Bao hilo, liliitia nguvu zaidi Yanga na dakika ya 11 almanusra beki ‘Bwana Harusi’ Nsajigwa Shadrack afunge bao, lakini shuti lake kali la mbali liliokolewa na kipa wa Bunamwaya, Muwonge Robert.
Baada ya kosakosa za hapa na pale, kiungo mpya wa Yanga, Rashid ‘Chiddy’ Gumbo, alifunga bao tamu dakika ya 39, kwa shuti la umbali wa zaidi ya mita 20 na kali lililomshinda kipa wa Bunamwaya.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Yanga, Mganda Samuel ‘Sam’ Timbe kumtoa beki Nsajigwa na kumuingiza winga Julius Mrope, yaliivuruga timu hiyo na kujikuta wakipigwa mabao mawili ya haraka haraka na wapinzani wao.
Alipoingia, Mrope alikwenda kuchukua nafasi ya Godfrey Taita wingi ya kulia, aliyerejea kwenye nafasi yake halisi, beki ya kulia, lakini haikumzuia mshambuliaji wa mabingwa wa Uganda, Owen Kasule, kufunga mabao dakika ya 61, akiunganisha pasi nzuri ya Kisaliita Ayub na dakika ya 75 akiwazidi ujanja mabeki wa Yanga.
Lakini wakati mashabiki wa Yanga wakiwa kama wamemwagiwa maji kwa kushuhudia timu yao ‘ikichomolewa’ mabao kiulaini, mshambuliaji wa zamani wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Davies Mwape ‘aliwatekenya’ na kuwainua vitini kwa bao tamu la ushindi dakika ya 92.
Tangu hapo, Uwanja wa Taifa uligubikwa na furaha, rangi za njano na kijani zikitawala kwa shangwe za kuingia Robo Fainali kama vinara wa kundi hilo. Tayari wapinzani wao, Simba walikuwa wamekwishajihakikishia kuingia Robo Fainali pia kwa ushindi wa mabao 2-0 juzi, dhidi ya Enticelles ya Rwanda.
Baada ya mchezo huo, Timbe, mwenye rekodi ya kutwaa mataji manne ya Kagame na klabu nne tofauti, SC Villa 2005, Polisi 2006, URA zote za Uganda 2007 na Atracao ya Rwanda 2009, alisema kwamba mechi ilikuwa ngumu, hasa kipindi cha pili.
“Walipoanza kurudisha mabao kipindi cha pili, nilikuwa namuomba Mungu japo tutoke sare ya 2-2, maana niliona kama wachezaji wangu wanazidiwa, lakini nashukuru kwa kazi nzuri aliyoifanya Mwape kwenye dakika za nyongeza,” alisema Timbe.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yew Berko, Nsajigwa Shadrack/Julius Mrope, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Bakari Mbegu, Nurdin Bakari, Godfrey Taita, Rashid Gumbo, Davis Mwape, Kiiza Hamisi na Kigi Makasi.
Bunamwaya: Muwonge Robert, Kimuli Robert, Kisaliita Ayub, Kavuma Habib, Seku Ronald, Muganga Ronard, Ssali Edward, Kasule Owen, Ssali Andy, Odur Tonny na Luwaga Kizito.

Comments