VUMI WA K-MONDO SOUND KUCHUANA NA TSHALA MUANA

MWANAMUZIKI wa kizazi kipya wa Tanzania, Vumilia  Abraham Mwaipopo “Vumi’ au Queen of the Night anatarajiwa kupambana na nguli wa muziki wa Mutuashi barani Afrika Elizabeth Modiakai ‘Tshala Muana’ katika tuzo za Afrika Mashariki zitakazofanyika baadae Agosti 20 mwaka huu mjini Nairobi Kenya.
Taarifa iliyotolewa juzi na waandaji wa tuzo hizo, kampuni ya Golden Dreams ya Nairobi, ilimtaja Vumi katika tuzo ya mwanamuziki bora wa muziki wa Rhumba sambamba na Tshala Muana na Masha Mapenzi wa Kenya.
Vumi ameingia katika kinyang’anyiro hicho kwa wimbo wake ambao unaendelea kutingisha kwenye anga la muziki Afrika Mashariki na Kati uitwao Tatizo Umasikini, wakati Tshala Muana ambaye alipata kuwa kiongozi wa umoja wa kinamama wa Chama kinachoongozwa na Rais Joseph Kabila wa Kongo ameingia kwenye tuzo hizo kwa wimbo wake uitwao Malozi huku Masha akiingia kwa kibao chake Kala Ulele.
Akizungumza baada ya kupata taarifa za kuchaguliwa kuingia kwenye fainali hizo, Vumi alisema amefurahishwa na hatua hiyo na kuomba wadau wampigie kura katika kinyanyang’anyiro hicho hasa ikizingatiwa anapambana na msanii gwiji huku pia akichuana na mwanamuziki mwingine kutoka Kenya ambako tuzo ndio zitafanyika.
“Kwa kweli nimefurahi na namshukuru Mungu, nawashukuru watu wote waliohusika katika kutengeneza wimbo huo, bendi yangu ya K-Mondo Sound, producer Alain Mapigo, Video Producer Hassan Kundamayi wa HK Vision, naomba sasa  waniunge mkono kwenye hatua inayofuata ya upigaji kura,” amesema.
Mbali ya Vumi lakini pia mwanamuziki wa bendi ya Akudo Impact, Christian Bella  naye ana kibarua kigumu kwani wimbo wake wa Yako wapi Mapenzi unapambana na Papa Wemba  kwa wimbo wake  wa Six Million sambamba na Fally Ipupa katika Sexy Dance.
Msondo ngoma wao wako kwenye kundi bora la Rhumba kwa wimbo wao Kalunde wakipambana na Wenge BCBG na Werrason. Jaydee naye ameingia mara mbili kwenye tuzo hizo wakati MwanaFA na AY wako kwenye best Collabo. Producre Hammer B amechaguliwa kuwa Jaji kwenye tuzo hizo. Albamu ya Tatizo umasikini pia inatarajia kuingia mtaani mwezi ujao.

Comments