UJIO WA HEARTS OF OAK, ASANTE KOTOKO BONGO WAOTA MBAWA


Dar es Salaam 8th Ijumaa, Julai 2011… mashindano ya soka ya kimataifa yajulikanayo kama Tanzania International Cup yaliyopangwa kufanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ya Julai 16-17 sasa yameahirishwa hadi itakapotangazwa tena.

Waandaaji wa mashindano hayo yanayoshirikisha miamba ya soka Simba na Yanga za Tanzania na Asante Kotoko na Hearts of Oak za Ghana wamesema wanahitaji muda zaidi kukamilisha maandalizi yao pamoja na wadau wengine ili kuyafanya mashindano kuwa yenye ubora unaotarajiwa. Waandaaji hao ni Lumuli Marketing na Octagon kutoka Afrika Kusini.

“Wawakishi kutoka Asante Kotoko na Hearts of Oak tayari wameshawasili jijini Dar es Salaam kusaini mkataba lakini tunadhani hatujawai tayari kufanya mashindano wiki ijayo kama tulivyotangaza awali hadi pale maandalizi yote yatakapokamilika.”,alisema Sidwell Jan, Mkurugenzi Mtendaji wa Lumuli Marketing.

Timu za Simba na Yanga ambazo hivi sasa ziko katika kinyang’anyiro cha kutwaa taji la michuano ya Kagame inayofanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam zimethibitisha kushirika mashindano ya uzinduzi ya Tanzania International Cup yatakayokuwa yanafanyika kila mwaka jijini.

Bw. Jan alisisitiza kuwa mashindano hayo yameahirishwa tu kwa muda lakini yatafanyika kama ilivyopangwa katika tarehe itakayotangazwa baadaye wakati mipango yote itakapokuwa imekamilika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Octagon Bonga Sebesho alisema kwa sasa wanakwenda kwenye nchi nyingine za Afrika kwa lengo hilo hilo na kusema kuwa watarudi Tanzania muda si mrefu kuja kukamilisha adhima yao ya kuzindua Tanzania International Cup. 

Comments