TIMU ZA LIGI KUU ZABISHA HODI TFF KUWAWEKEA WACHEZAJI PINGAMIZI


Klabu tatu za daraja la kwanza zimeliandikia Shirikisho la Mpira wa Miguu 
Tanzania (TFF) zikiweka pingamizi kwa wachezaji wao waliosajiliwa katika klabu 
nyingine za Ligi Kuu ya Vodacom.
 
Polisi Morogoro inapinga wachezaji wake Majaliwa Shabani Mbaga, na Shomari 
Kapombe ambaye Simba imemuombea usajili kusajiliwa na timu nyingine kwa vile 
bado ina mkataba na wachezaji hao.
 
Nayo Majimaji ya Songea imeweka pingamizi kwa wachezaji wake kumi na moja (11) 
inaosema kuna tetesi kuwa wamesajiliwa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya 
Vodacom, lakini hawajafanyiwa taratibu za uhamisho ingawa bado wana mikataba na 
timu hiyo.
 
Wachezaji hao ni Said Mohamed (Yanga), Juma Mpola, Evarist Maganga, Kulwa Mobby, 
Ally Bilaly (Villa Squad), Mohamed Mpola, Paul Ngalema, Lulanga Mapunda, Hamad 
Waziri, Yahya Shaban Haruna na Ulimboka Mwakingwe (Simba).
 
Kwa upande wa AFC ya Arusha kupitia kwa Mwenyekiti wake Peter Temu imesema hadi 
siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji- Julai 15 mwaka huu hakuna mchezaji wake 
aliyekuwa ameombewa uhamisho kujiunga na timu nyingine.
 
Hivyo inaweka pingamizi kwa wachezaji wote wenye mikataba na klabu hiyo 
kusajiliwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom, na kwa mchezaji atakayekuwa 
amesajiliwa si halali kwa vile uhamisho wote ni lazima uidhinishwe na Mwenyekiti 
wao.
 
Boniface Wambura 
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Comments