TFF YAPONGEZA MAFANIKIO YA KOMBE LA KAGAME

BONIFACE WAIMBURA, OFISA HABARI WA TFF
Michuano ya kuwania Kombe la Kagame iliyofanyika nchini kuanzia Juni 25 hadi
Julai 10 mwaka huu imekwenda vizuri huku timu za Tanzania, Yanga na Simba
zikifanya vizuri kwa kufika hatua ya fainali. TFF tunazipongeza timu hizo kwa
uwakilishi mzuri ziliotupa, hasa Yanga kwa kuibuka mabingwa.

Shukrani za pekee tunatoa kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mechi za
michuano hiyo zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro. Mahudhurio ya washabiki katika mechi zote yaliingiza
jumla ya sh. bilioni 1.073. Fedha hizo zimetuwezesha kulipia gharama zote za
mashindano.
 Pia tunatoa shukrani kwa wadau wengine waliowezesha mashindano hayo kufanikiwa
wakiwemo wadhamini, hoteli, kampuni za usafiri, ulinzi, Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, waandishi wa habari Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) na klabu ya TCC Chang’ombe kwa kutoa viwanja vya mazoezi na Serikali kwa
kutoa Uwanja wa Taifa.
 Hoteli hizo ni Safina, Landmark, Lunch Time, Marriot, Paradise City, Valentino,
Spice Inn, Blue Pearl, Akubu na Jangwani Plaza za Dar es Salaam. Oasis, Top Life
na Kingston za Morogoro.,
Licha ya mafanikio hayo, tunawaomba radhi mashabiki kutokana na kukatika umeme
kwenye Uwanja wa Taifa baada ya mechi ya fainali kati ya Yanga na Simba. Tukio
hilo lilitokea wakati wa kukabidhi zawadi kwa timu mbalimbali zilizofanya vizuri
katika mashindano hayo.

Comments