TFF YAANIKA MAJINA YA WACHEZAJI WA TIMU ZA LIGI KUU WALIOHAMISHWA KUTOKA TIMU MOJA KWENDA NYINGINE

Uhamisho wa wachezaji wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2011/2012 ulifikia tamati jana 
saa 6 kamili usiku. Wachezaji ambao maombi yao ya uhamisho yamewasilishwa TFF ni 
Shabani Kado kutoka Mtibwa Sugar kwenda Yanga, Salum Machaku kutoka Mtibwa Sugar 
kwenda Simba na Idrisa Rajab kutoka African Lyon kwenda Yanga.
 
Hao ni kwa wachezaji ambao maombi yao yametumwa kwa njia ya barua. Kwa vile 
uhamisho vile vile unaweza kufanywa kwa njia ya mtandao (Transfer Match System- 
TMS), uhamisho mwingine uliofanyika utafahamika kesho baada ya Kurugenzi ya 
Mashindano kupitia mfumo huo wa TMS ambao klabu zote za Ligi Kuu tayari zina 
namba zao maalumu za kuingia (passwords).
 
WACHEZAJI WALIOTOLEWA KWA MKOPO
Wachezaji waliotolewa kwa mkopo kutoka Simba kwenda klabu zingine ni Aziz Gilla 
na Mbwana Bakari (Coastal Union), Mohamed Kijuso, Mohamed Banka na Haruna Shamte 
(Villa Squad), Meshack Abel (Ruvu Shooting), Juma Jabu, Andrew Kazembe, Paulo 
Terry na Godfrey Wambura (Moro United).
 
Kutoka Azam ni Sino Augustino na Selemani Kassim ambao wanakwenda African Lyon, 
na Tumba Louis (Moro United). Yanga imewapeleka wachezaji wake Omega Seme na Idd 
Mbaga kwa mkopo African Lyon.

Comments